Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne tarehe 13 Agosti 2013 amekutana na viongozi pamoja
na wachezaji wa timu za taifa kutoka Italia na Argentina wanaojiandaa kwa ajili ya
kucheza mechi ya kirafiki mjini Roma hapo tarehe 14 Agosti 2013.
Akizungumza
na wanamichezo hao, Baba Mtakatifu amekazia kwa namna ya pekee kabisa umuhimu wa kudumisha
urafiki katika michezo, kwani kuna umati mkubwa wa watu wanaowafuata wanapokuwa wakitandaza
kabumbu uwanjani na hata nje ya viwanja vya michezo.
Hii ni dhamana na wajibu
mkubwa kwa wanamichezo. Michezo haina budi kujikita katika: uzuri, majitoleo na urafiki,
ikiwa kama mambo haya yanayokosekana uwanjani hapo kuna patashika nguo kuchanika.
Katika michezo ubinafsi hauna budi kuwekwa kando ili kujenga moyo na mshikamano wa
timu unaosimikwa katika ari, na moyo wa kupenda na kufurahia michezo na wala si kwa
sababu ya fedha.
Baba Mtakatifu anasema, wachezaji wa kitaifa na kimataifa
hawana budi kujenga na kukuza moyo wa kupenda michezo, jambo ambalo ni jema katika
maisha ya kijamii, daima wakitafuta mafao ya wengi yanayojikita zaidi na zaidi katika
majitoleo, moyo na uzuri wa michezo.
Wanamichezo wanakumbushwa kwamba, kabla
ya kuwa ni watu mashuhuri, wao ni binadamu, wenye karama na mapungufu; mawazo, matumaini
na matatizo yao. Hata kama ni mabingwa na watu mashuhuri katika michezo, wanapaswa
bado kuendelea kubaki kuwa ni watu katika michezo na maisha. Ni watu wanaobeba utu.
Baba
Mtakatifu amewataka viongozi wa michezo kutambua umuhimu wa michezo badala ya kugeuza
michezo kuwa ni biashara. Ni wajibu wao kuhakikisha kwamba, watu wanapenda na kufurahia
michezo ili hatimaye, kuondokana na tatizo la ubaguzi wa rangi unaojitokeza mara
kwa mara kwenye viwanja wa michezo. Wanamichezo wakizingaztia dhamana yao, michezo
inakuwa ni fursa ya kuwatajirisha watazamaji na wapenda michezo. Ni mwelekeo unaoweza
pia kuondoa uhalifu kwenye michezo na watu kuanza kujisikia kuwa ni watoto wa familia
moja.
Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha wanamichezo hao kwamba, alipokuwa
kijana mdogo mwenye umri wa miaka kumi hivi, alikuwa anakwenda kuangalia mpira na
daima alipokuwa anarudi nyumbani alikuwa ni mtu aliyesheheni furaha. Amewashukuru
wanasoka na viongozi wao kutoka Argentina. Amewakumbusha kwamba, wanamichezo ni kioo
cha jamii na mfano bora wa kuigwa na vijana wengi kwani wana karama na vipaji vinavyomwilishwa
katika maisha.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, ana matumaini na wanamichezo
kwa mambo mengi wanayoweza kutenda kwa ajili ya kuwasaidia vijana. Watu wengi wanawaonea
wivu, lakini watambue kwamba, wanaweza kuwa ni mfano bora wa kuigwa au wakabezwa na
Jamii kutokana na matendo yao. Baba Mtakatifu anawataka wanamichezo kuwa ni mfano
wa ukweli na heshima kwa wengine.