Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana linawataka waamini na wananchi wenye mapenzi mema
kuendelea kudumisha misingi ya haki, amani, utulivu, upendo na mshikamano wa kitaifa,
wakati huu Mahakama kuu inapojiandaa kutoa hukumu ya rufaa ya kupinga matokeo ya uchaguzi
mkuu uliofanyika nchini humo Desemba, 2012.
Kwa mara ya kwanza katika historia
ya Ghana, Mahakama kuu imekubali kusikiliza rufaa iliyotolewa na vyama vya upinzani
vilivyokataa kukubali matokeo ya uchaguzi mkuu nchini humo yaliyokuwa yamempatia ushindi
Rais John Dramani Mahama. Mahakama ilianza kusikiliza kesi hii ya kihistoria tangu
tarehe 16 Aprili 2013 na kumaliza kukusanya ushahidi wote hapo tarehe 17 Julai 2013.
Mahakama kuu inatarajiwa kutoa hukumu ya kesi hii mwishoni mwa Mwezi Agosti 2013.
Baraza
la Maaskofu Katoliki katika mkutano wake uliohitimishwa hivi karibuni, linawataka
wananchi katika kipindi hiki kigumu na tete kujenga na kuimarisha amani na mshikamano
wa kitaifa kwani ikiwa kama hawataweza kuwa makini, maafa makubwa yanaweza kutokea
nchini Ghana. Amani na utulivu vidumishwe kabla, wakati na baada ya Mahakama kuu kutoa
hukumu ya kesi hii ya kihistoria, inayoiweka Ghana katika njia panda.
Maaskofu
Katoliki Ghana wanaendelea kuwahimiza waamini na wananchi katika ujumla wao, kuhakikisha
kwamba, wanashiriki kikamilifu katika ujenzi wa misingi ya haki, amani, utulivu na
upatanisho wa kitaifa. Itakumbukwa kwamba, Ghana ilifanya marekebisho ya Katiba yake
kunako mwaka 1992 na imeongoza chaguzi kuu mara sita na kwa mara ya kwanza, matokeo
ya uchaguzi mkuu yamepingwa Mahakamani, kielelezo cha ukomavu wa kisiasa na kidemokrasia.
Katika
hali hii tete nchini Ghana, vyombo vya mawasiliano ya Jamii vina mchango mkubwa wa
kuhakikisha kwamba, vinasaidia mchakato wa kuimarisha amani, upendo, mshikamano na
upatanisho wa kitaifa. Vyombo vya ulinzi na usalama vitekeleze wajibu wake kwa ajili
ya mafao ya wengi. Kwa wale watakaobahatika kutangazwa kuwa ni washindi, watambue
dhamana na changamoto iliyoko mbele yao katika ujenzi wa demokrasia shirikishi, wajibu
na dhamana ya kusimama kidete kupambana na rushwa, ufisadi na ukosefu wa fursa za
ajira miongoni mwa vijana, kwani haya ni kati ya matatizo makubwa yanayowakabili wananchi
wa Ghana kwa wakati huu.
Maaskofu Katoliki Ghana wanasema, kwamba, amani ni
zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomshikirisha mwanadamu. Wananchi hawana budi
kuhakikisha kwamba, wanajifunza namna ya kulinda na kutunza zawadi ya amani kwa ajili
ya mafao na ustawi wa nchi yao. Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana
kwamba, Mahakama kuu itatekeleza wajibu wake kwa kuzingatia misingi ya ukweli na haki
wakati wa kutoa hukumu.