Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 850 ya Kanisa kuu Notre Dame, Paris
Kardinali Andrè Vingt Trois, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Paris, Ufaransa anatarajiwa
kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kilele cha Maadhimisho ya Jubilee ya
Miaka 850 tangu kujengwa kwa Kanisa kuu la Notre Dame, Jimbo kuu la Paris sanjari
na Siku kuu ya Kupalizwa mbinguni Bikira Maria, hapo tarehe 15 Agosti 2013.
Sherehe hizi
zinatanguliwa na siku mbili za Maadhimisho, kuanzia tarehe 14 Agosti 2013 kwa Maandamano
makubwa ya mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Katika mkesha wa Siku kuu
ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni, majira ya jioni waamini na mahujaji watafanya
maandamano kwenye Meli, Boti na Mashua kuzunguka Mto Senna, ulioko mjini Citè na St.
Louis.
Waamini na mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia watapata fursa
pia ya kuangalia maonesho ya picha zilizochorwa kunako karne ya XVII, kuhusiana na
maisha ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Picha hizi zimeendelea kuhifadhiwa
kwenye Kanisa kuu la Notre Dame, Jimbo kuu la Paris kutokana na utashi ulioneshwa
na Mfalme Louis XIII aliyeiweka nchi ya Ufaransa chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira
Maria kunako mwaka 1638.