Jubilee ya miaka 200 ya kukamilika kwa Ujenzi wa Kanisa kuu la Jimbo kuu la Mexico
City
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Kardinali Norberto Rivera Carrera
wa Jimbo kuu la Mexico City, nchini Mexico, wakati huu wanapoadhimisha Jubilee ya
miaka 200 tangu kukamilika kwa ujenzi wa Kanisa kuu Jimboni humo, hapo tarehe 15 Agosti
2013, anasema, ni changamoto kubwa ya kukuza ari na mwamko wa kimissionari. Waamini
watumie fursa hii kuimarisha imani, matumaini na mapendo na vijana waendelee kufurahia
zawadi ya imani.
Baba Mtakatifu anawaambia waamini wa Jimbo kuu la Mexico
City kwamba, Maadhimisho ya Jubilee hii yanafumbata utajiri na amana kubwa ya maisha
ya kiroho. Iwe ni fursa ya toba na wongofu wa ndani, kila mwamini akijitahidi kutekeleza
dhamana na wajibu wake katika maisha na utume wa Kanisa kama Mbatizwa, tayari kujitosa
kimasomaso kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa ari na nguvu mpya ya kimissionari.
Baba
Mtakatifu anasema kwamba, waamini katika Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu
wanajichotea nguvu ya kuweza kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake,
kwa njia ya upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Ni mwaliko
wa kujenga na kuimarisha matumaini kwa ajili ya kesho iliyo bora zaidi bila kutoa
mwanya kwa baadhi ya watu wanaotaka kupokonya matumaini haya kutoka katika mioyo ya
waamini.
Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini wa Jimbo kuu la Mexico
City, kuhakikisha kwamba, Neno la Mungu linalotangazwa wakati wa Ibada mbali mbali
linajikita katika mioyo na maisha ya watoto na vijana ambao ni mlango wa furaha na
matumaini kwa Kanisa na Jamii. Vijana wapewe na kurithishwa imani na tunu msingi za
maisha ya Kikristo na kiutu, kwa kutambua kwamba, Yesu Kristo ni Mkombozi na Rafiki
mwema, kamwe hawezi kuwaacha katika utupu!
Baba Mtakatifu anaendelea kuwahimiza
wazazi na walezi kuhakikisha kwamba, wanatekeleza kwa dhati dhamana waliyokabidhiwa
na Mama Kanisa na Jamii katika malezi na makuzi ya watoto wao, si tu kwa kutegemea
nguvu zao binafsi bali pia kwa neema na baraka za maisha ya sala.
Baba Mtakatifu
Francisko anahitimisha ujumbe wake wa matashi mema wakati huu Jimbo kuu la Mexico
City linapoadhimisha Jubilee ya miaka 200 tangu kukamilika kwa ujenzi wa Kanisa kuu
la Jimbo kuu la Mexico City kwa kuwaweka waamini wote chini ya ulinzi na usimamizi
wa Bikira Maria wa Guadalupe.