2013-08-13 07:22:25

Japan na Tanzania kushirikiana kuelimisha wataalam wa Nishati


Japan imeahidi kuwapa mafunzo watanzania 1,000 juu ya uzalishaji wa nishati ya umeme ili kuiwezesha Tanzania kupata wataalamu wake wenyewe kwenye sekta ya nishati ya umeme.
Mafunzo haya yataanza rasmi mwezi Januari mwaka 2014 kama ilivyobainishwa na Waziri wa Uchumi, Biashara na Viwanda wa Japan Bwana Toshimitsu Motegi kwenye semina ya siku moja kati ya Tanzania na Japan. Seminar hiyo, iliyowakutanisha wafanyabiashara 200, makampuni 13 ya kibiashara na mengine matano ya Kiserikali kutoka nchini Japan ambayo imefanyika mwishoni mwa Juma, Jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Ahadi hiyo imefuatia mazungumzo kati ya Serikali hizi mbili, Tanzania ikiwakilishwa na Waziri wake wa Nishati na Madini, Prof Sospeter Muhongo, ambapo kulifikiwa makubaliano juu ya kukuza mafunzo ya wataalam wa mambo ya nishati na uzalishaji wa nguvu za umeme nchini Tanzania.
Waziri Motegi anasema, Serikali ya Japan itachangia zaidi katika kukuza soko la ajira miongoni mwa vijana Barani la Afrika. Japan inakadiria ongezeko la wafanyakazi kwenye makampuni ya Kijapani kutoka 200,000 hadi 400,000 kwa kipindi cha miaka mitani ijayo. Amewaomba wananchi wa Tanzania kuchukua fursa hii ili kufaidi kutokana na mafunzo yanayotolewa na serikali yake kupitia shirika la Nguvu kazi watu na Maendeleo ya viwanda, HIDA, ili kujenga uwezo wa kuendesha shughuli kwenye sekta ya nishati.
Semina hiyo ilifunguliwa na Waziri wa Biashara na Viwanda Dak. Abdalla Kigoda ambaye aliitaka serikali ya Japan kukifungua tena kiwanda cha High Precision Technology Centre kilichofunguliwa jijini Dar es Salam 1981 na hatimaye kulikunja jamvi la kazi zake kunako mwaka 1995.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe naye amesema kuwa semina hiyo ilikuwa na lengo la kutafuta upenyo wa kibiashara kwa makampuni ya mataifa haya mawili yakizingatia hasa ukuzaji wa sekta za reli, bandari na miundombinu nyingine za uchukuzi.
Semina hii ilitokana na maazimio yaliyoafikiwa kwenye mkutano wa Tano wa Kimataifa juu ya Maendeleo ya Afrika uliofanyika mjini Tokyo, Japan mwezi Juni, 2013 na ambao uliwahusisha marais wa mataifa 40 ya kiafrika. Semina ya Dar es Salam ilihudhuriwa pia na Rais Jakaya Kikwete ambaye aliishukuru Japan kwa kuandaa semina hiyo.








All the contents on this site are copyrighted ©.