2013-08-12 11:46:13

Wawekezaji kutoka Barani Afrika wanazidi kuongezeka!


Waafrika wanaendelea kujikita kwenye kinyang’anyiro cha kuwekeza Barani Afrika kinyume na fikira kwamba ni wawekezaji kutoka ulaya, Marekani na bara Asia pekee yao ndio wanaofaidika kwenye kinyang’anyiro hicho. RealAudioMP3

Waafrika wengi sasa nao wamevutiwa na ustawi wa kiuchumi na wanachukua fursa hiyo kujibwaga uwanjani ili kuweza kujiendeleza na kuchangia kukua kwa uchumi Barani Afrika. Mwelekeo wa uchumi, mikakati ya maendeleo endelevu na ongezeko la idadi ya vijana, vimewavutia wawekezaji nchini Afrika Kusini, Kenya, Nigeria na hata Namibia.

Kati ya Mwaka 2003 na 2011 uwekezaji Barani Afrika ulikuwa kwa asilimia 23%. Kiasi hiki ni kikubwa zaidi ya kile cha wawekezaji kutoka nje ya Bara la Afrika, na mara nne ya uwekezaji unaofanywa na mashirika yasiyo na asili ya kiafriKa.

Hivi karibuni Waziri wa Fedha wa Nigeria aliwaambia washiriki kwenye mkutano wa kimataifa wa Uchumi wa Afrika, inasikitisha kwamba mikutano ya aina hii hulenga hasa wawekezaji kutoka nje, ni wakati wa kuwalenga Waafrika wanaowekeza Barani Afrika pia. Ni dhahiri kwamba, uwekezeji wa kuvuka mipaka Barani Afrika unaongezeka kutokana na watu na makundi mbalimbali kutafuta masoko mapya ya kuwekeza nje ya nchi zao wenyewe, jambo ambalo litachangia sana maendeleo ya bara hili.

Ikumbukwe kwamba, Bara la Afrika lina rasilimali na maliasili nyingi, lakini uchumi wake bado umedoda. Ifikiapo Mwaka 2030, Afrika itakuwa na idadi ya watu bilioni 1.2, kutoka milioni 500 wakati huu. Afrika ina idadi kubwa ya vijana wanaoweza kuchangia katika mikakati ya uzalishaji, ikiwa kama watawezeshwa kikamilifu.

Huu ni wakati muwafaka kwa mashirika ya kiafrika kuweza kuwekeza ndani na nje ya nchi asilia na kufaidi kutokana na ushirikiano na wawekezaji kutoka nje ili waweze kujifunza na kukuza uchumi na ustawi wa bara la Afrika ambalo linaonekana kubaki nyuma katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Kwa sasa Afrika kusini inangoza kwa uwekezaji wa ndani ya nchi na Barani Afrika kwa jumla.

Nigeria pia haijaachwa nyuma kwani mashirika yake kama vile Benki ya Muungano wa Afrika na Dangote Cement, inayomilikiwa na tajiri mkubwa zaidi wa Afrika, Aliko Dangote, yameweza kuwekeza kwenye nchi mbalimbali Barani Afrika zikiwemo Cameroon, Kenya, Tanzania, Ghana na Msumbiji.

Uchumi wa Afrika pia utafaidika kutokana na sekta ya nishati ya gas na mafuta ya petroli ambayo itaendelea kukua kwa miaka kumi ijayo. Hivyo basi, ni matumaini ya wengi kwamba rasilimali za Afrika zitaendelea kuwa chanzo cha baraka kwa Bara hili ambalo kwa bahati mbaya limekumbwa na kinzani, vita, magonjwa, njaa, umaskini, uchu wa mali na madaraka pamoja na sera potofu za matumizi ya rasilimali ya Bara la Afrika.

Umefika wakati kwa viongozi na watunga sera barani Afrika kutoa kipaumbele cha kwanza katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi badala ya kukumbatia ubinafsi na uchu wa mali unaoyatumbukiza mataifa mengi katika migogoro na vita.
All the contents on this site are copyrighted ©.