2013-08-12 09:44:20

Wanasoka wa Italia na Argentina kukutana na Papa Francisko, Jumanne, 13 Agosti 2013


Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne tarehe 13 Agosti 2013 anatarajiwa kukutana na kuzungumza na wachezaji wa Timu za Taifa la Italia na Argentina, wanaotarajiwa kutandaza kabumbu kwa heshima ya Baba Mtakatifu Francisko ambaye kwa asili ni mshabiki mkubwa wa mpira.

Taasisi ya Kipapa ya Sayansi, itatumia fursa hii kuanzisha majiundo makini yanayopania kutoa nafasi kwa Jamii kuweza kuwashirikisha watu wengi zaidi katika maisha na vipaumbele vyake; kila mtu akipewa nafasi ya kukuza na kuendeleza karama na vipaji ambavyo amekirimiwa na Mwenyezi Mungu mintarafu utamaduni, imani, tunu msingi za kiutu pamoja na utunzaji bora wa mazingira.

Marafiki wa Baba Mtakatifu Francisko wamekubaliana kimsingi kwamba, kabumbu litakalosakatwa kati ya Italia na Argentina katika siku itakayopangwa, iwe ni fursa ya kuanzisha mradi wa mchakato wa mshikamano unaopania kuwashirikisha vijana wengi katika elimu inayozingatia udugu na mshikamano kati ya watu.







All the contents on this site are copyrighted ©.