2013-08-12 09:28:58

Upendo wa Mungu una jina na sura kamili, yaani Yesu Kristo!


Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake wakati wa sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili iliyopita, tarehe 11 Agosti 2013, kwenye Uwanjwa wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, alikazia umuhimu wa waamini kuhakikisha kwamba, mioyo yao inakesha tayari kukutana na Kristo, hamu kuu ya waamini. Hii inatokana na ukweli kwamba, katika kila moyo wa mwanadamu kuna hamu iliyofichika ndani mwake.

Yesu alipokuwa njiani kwenda Yerusalem pamoja na wafuasi wake, ili kuweza kukabiliana uso kwa uso na Fumbo la Msalaba, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake, aliwaangalisha kutokukumbatia mno mali ya ulimwengu na badala yake kuwa na imani kwa Mwenyezi Mungu, daima wakiwa tayari kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Kwa Yesu hii ilikuwa ni hatua muhimu ya Maandalizi ya kurudi nyumbani kwa Baba.

Kwa Wakristo wa nyakati hizi, wanaendelea kungojea pale Yesu atakaporudi ili kuwachukua na hatimaye, kuwashirikisha furaha ya uzima wa milele kama alivyofanya kwa Bikira Maria kupalizwa mbinguni, mwili na roho. Hii inaonesha kwamba, Mkristo katika undani wa maisha yake anabeba hamu ya kutaka kukutana na Kristo akiwa pamoja na wenzi wa hija ya maisha yake hapa duniani.

Yesu alikwisha waambia kwamba, "kwa kuwa hazina yenu ilipo, ndipo itakapokuwapo na mioyo yenu" Lk. 12:34. Hamu hiyo ambayo iko moyoni mwa kila mwamini anasema Baba Mtakatifu Francisko inawabidisha waamini kutaka kukutana na Kristo ambaye ni chemchemi ya maisha na furaha ya kweli. Ni hamu ya kutaka kutenda kwa ajili ya kuwasaidia wengine, kila mtu kadiri ya wito na maisha yake, kwa kutambua kwamba, Mungu ni Upendo.

Baba Mtakatifu anasema, upendo kwa Mungu na jirani unamwezesha mwamini kuweza kukabiliana na changamoto za maisha ya kila siku. Upendo wa Mungu una jina na sura kamili yaani Yesu Kristo, ambaye ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo ambayo ni zawadi ya Mungu kwa binadamu. Nguvu ya upendo wa Mungu inathamanisha na kuimarisha tunu msingi za maisha ya kifamilia, uwajibikaji na tija sehemu za kazi; ufanisi katika masomo, katika ujenzi wa urafiki; ni upendo unaojionesha katika sanaa na katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, upendo wa Mungu unawajengea waamini uwezo wa kukabiliana pia na kinzani na changamoto za maisha, kwa kuwa na matumaini ya kuendelea na hija ya maisha ya uzima wa milele. Dhambi na mapungufu ya binadamu yanapata tiba kwa njia ya Yesu Kristo aliyempatanisha Mungu na mwanadamu aliyekuwa anaogelea katika dimbwi la dhambi na mauti.

Baba Mtakatifu amewakumbusha waamini kwamba, tarehe 11 Agosti, Mama Kanisa alikuwa anafanya kumbu kumbu ya Mtakatifu Klara wa Assisi aliyefuata nyayo za Mtakatifu Francisko wa Assisi akaacha yote kwa ajili ya kujitosa kimasomaso katika maisha ya kuwekwa wakfu, akamwilisha ndani mwake, Nadhiri ya Ufukara, kielelezo makini cha ujumbe wa Injili, Jumapili ya kumi na tisa ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa.

Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Bikira Maria ili aweze kuwasaidia kadiri ya mafundisho ya Kristo kila mwamini kadiri ya wito na maisha yake ndani ya Kanisa.







All the contents on this site are copyrighted ©.