Familia ina dhamana ya kurithisha imani ya Kikristo kwa watoto wake!
Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil, limeanza Maadhimisho ya Juma la Familia Kitaifa,
litakalohitimishwa hapo tarehe 17 Agosti 2013 kwa kuongozwa na kauli mbiu "Urithishaji
na elimu ya imani ya Kikristo katika Familia". Mababa wa mkutano mkuu wa Aparecida
walibainisha kwamba, Familia ni kati ya zawadi kubwa ambayo Mwenyezi Mungu amewakirimia
wananchi wa Amerika ya Kusini.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake
kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil wakati huu wa Maadhimisho ya Juma la Familia
Kitaifa, anapenda kuchukua fursa hii kwanza kabisa kuwashukuru kwa mapokezi makubwa
waliyomwonesha wakati wa hija yake ya kichungaji nchini Brazil sanjari na Maadhimisho
ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani huko Rio de Janeiro.
Baba Mtakatifu anawaalika
kwa namna ya pekee, wazazi na walezi kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na utume
wao ndani ya Familia, kwa kutambua kwamba, wao ni wadau wa kwanza wanaoshirikiana
na Mwenyezi Mungu katika malezi na makuzi ya watoto wao kwa sasa na kwa siku za usoni.
Kutokana na dhamana hii, wazazi na walezi wanayo dhamana kubwa ya kuhakikisha kwamba,
wanajenga na kudumisha misingi ya imani kama sehemu ya mchakato wa ukomavu wa imani
miongoni mwa watoto wao.
Wazazi na walezi walirthishe imani hii kwa njia ya
maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili na matakatifu; kwa kutambua
na kuenzi kweli msingi za maisha kadiri ya upendo na mpango wa Mungu katika maisha
ya mwanadamu; watoto wasaidiwe kupata mwanga na ufunuo wa Mungu katika hija ya maisha
yao. Katika ulimwengu wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani,
wazazi wawasaidie watoto wao kutambua na kuthamini zawadi ya maisha inayopaswa kulindwa
tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida yanapomfika
kadiri ya mpango wa Mungu.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, watoto ni zawadi
kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, Jamii inawajibu wa kuwatunza na kuwasaidia wazee
katika safari ya maisha yao hapa duniani, kwani wazee ni amana ya Jamii, wanamiliki
utajiri mkubwa na hekima ambayo wanapaswa kuwarithisha vijana wa kizazi kipya. Ni
matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Brazil itaendelea kusimama kidete kulinda na kutetea
upendo unaorutubishwa kwa njia ya imani kama kito cha thamani kutoka kwa Mwenyezi
Mungu.
Mwishoni, Baba Mtakatifu anazikumbuka na kuziombea Familia nchini Brazil
kwa kuziweka chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria wa Aparecida.