Waamini wote wana dhamana ya kulinda na kutunza mazingira!
Waislam, Wakristo na waamini wa dini mbali mbali nchini Niger, wanayo dhamana kutekeleza
wajibu wao kama watumishi waaminifu kwa Mwenyezi Mungu, muumba wa mbingu na dunia,
daima wakijitahidi kulinda na kutunza mazingira, zawadi ya Mungu inayomjalia mwanadamu
furaha ya kweli.
Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Niger
kwa waamini wa dini ya Kiislam wakati huu wanapoendelea kusherehekea Siku kuu ya Id
El Fitri iliyohitimisha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, Kipindi cha kusali,
kufunga na kutoa sadaka kwa maskini. Wakati huu wananchi wengi nchini Niger wako mashambani
kuvuna matunda ya jasho la mikono yao. Ni muda wa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya mvua
na mavuno mazuri kwa mwaka 2013.
Baraza la Maaskofu Katoliki Niger linawaalika
waamini wa dini mbali mbali nchini humo kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kushirikiana
vyema na mpango wa Mungu katika kulinda na kutunza mazingira badala ya kuelemewa na
ubinafsi ambao ni chanzo kikuu cha uharibifu wa mazingira kwa kizazi cha sasa na kile
kijacho.
Waamini waendelee kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema katika
kulinda na kutunza mazingira, kwa kutambua kwamba, huu ni wajibu wao msingi. Dhamana
hii wanapaswa pia kuwarithisha vijana wa kizazi kipya ili wajenge utamaduni wa kuheshimu
na kuhifadhi mazingira.
Baraza la Maaskofu Katoliki Niger, linawatakia kheri
na baraka tele Waamini wa dini ya Kiislam wanapo endelea kuadhimisha Siku kuu ya Id
el Fitri kwa mwaka 2013. Kiwe ni kipindi cha neema na baraka, amani na utulivu unaobubujika
kutoka katika miyo ya waamini, ili kujenga na kuimarisha upendo na mshikamano wa kitaifa.