2013-08-10 07:43:09

Vipaumbele: Vijana, Maskini na Kanisa


Baba Mtakatifu Francisko ameacha alama za kudumu alipokuwa Rio de Jenairo kwenye maadhimisho ya Siku ya 28 ya vijana Duniani. Ndivyo anavyoandika kwenye mtandao wa Baraza la Maaskofu Katoliki, Brazil, Kardinal Odilo Pedro Scherer, Askofu Mkuu wa Jimbo la Sào Paolo. RealAudioMP3

Alama alizoacha Baba Mtakatifu Francisko ni nyingi ila Kardinale Odilo Pedro anagusia hasa alama tatu zilizopewa kipaumbele cha kwanza na Papa Francisko: vijana, maskini na Kanisa.

Kwanza kabisa Vijana wa kizazi kipya ndio waliokuwa wahusika wakuu na sababu ya Baba Mtakatifu Francisko kwenda Brazil, ambako alikwenda kama Baba wa vijana wote, ili kukutana na kuwaonjesha mapendo, pamoja na kuendelea kuwatia moyo kusonga mbele kwa imani na matumaini kwa Kristo na Kanisa lake. Nao vijana waliitikia mwito wake kwa furaha kuu, wakazijaza barabara za Rio na ufuko wa Copacabana kwa furaha na imani – furaha iliyoje!

Na kuhusu maskini, Baba Mtakatifu alionyesha mshikamano wake na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Alionesha moyo wa heshima, ukarimu na hali ya kuguswa alipokuwa anazungumzia kuhusu umaskini wa hali na kipato, unaoendelea kumwandama mwanadamu katika hija ya maisha yake hapa duniani. Baba Mtakatifu alikazia umuhimu wa waamini na watu wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo.

Watu hasa waliguswa na moyo wa kujali alioonesha Baba Mtakatifu kwa wagonjwa na wenye mateso hasa alipotembelea hospitali na kitongoji duni cha Varginha. Aliwashukuru wananchi wa Brazil kwa moyo wao wa ukarimu na makaribisho mazuri waliomuonesha na akawaomba kusimama kidete ili kuweza kuyashinda matatizo ya kijamii yanayoikumba nchi yao.

Aliwaomba wote waliokuwa wakimsikiliza waepukane na uchu wa mali na madaraka, kwani furaha ya kweli haitokani na vitu alivyo nayo mtu, bali utu wake, furaha na amani ya ndani; hivyo waongozwe na moyo wa kiasi pasi ya kupenda makuu!

Kuhusu Kanisa; anaendelea kusema Kardinali Scherer kuwa, Baba Mtakatifu anaendelea kulihamasisha Kanisa kuwasikiliza vijana wake ili liweze kuwafikishia Habari Njema ya Wokovu pamoja na ile furaha ya imani.Baba Mtakatifu anaendelea kuwahimiza viongozi wa Kanisa kwenda pembezoni mwa Jamii na maisha ya watu, kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya na mwamko wa kimissionari kwa nyakati hizi.


All the contents on this site are copyrighted ©.