2013-08-10 08:59:46

Vijana wapewe elimu na malezi bora!


Sr. Maria Eugenia Thomas, Mama Mkuu wa Shirika la Masista wa Kazi ya Roho Mtakatifu katika mahojiano na Radio Vatican anasema kwamba, vijana ni tumaini la Kanisa na Jamii kwa ujumla. RealAudioMP3

Jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, kuna kundi kubwa la vijana wanaokimbilia mijini kutafuta riziki ya maisha, lakini mazingira wanamoishi ni hatari na ya kukatisha tamaa kiasi kwamba, vijana wanakosa dira na mwelekeo katika maisha.

Majiundo na malezi makini ni muhimu sana kwa vijana, ili kuwajengea uwezo wa kushiriki kikamilifu katika ustawi na maendeleo ya Jamii zao. Elimu ni ufunguo wa maendeleo na matumaini kwa vijana, lakini kuna haja ya kuwezeka na kuboresha zaidi mfumo wa elimu nchini Tanzania ili vijana waweze kuelimishwa barabara, kwani wao ni matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Shule za kata au sekondari zisiwe ni "mazizi" ya kuwakusanyia wanafunzi, bali mahali maalum pa vijana kuweza kupata: ujuzi, maarifa, maadili na utu wema. Hii ni changamoto kwa wadau mbali mbali wa elimu nchini Tanzania, kuhakikisha kwamba, wanafanya maboresho makubwa katika mfumo wa elimu, kwani matokeo ya mitihani ya hivi karibuni ni aibu kubwa kwa taifa linalotaka kuwekeza kwa vijana. Walimu wanapaswa kutambua dhamana na wajibu wao katika malezi na makuzi ya vijana wanapokuwa shuleni. Watambue kwamba, wana mchango mkubwa katika utoaji wa majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya. .

Sr. Maria Eugenia Thomas anasema kwamba, watanzania wengi ni watu wa kawaida kumbe, hawana uwezo wa kuwapeleka watoto wao katika shule za binafsi. Vijana popote pale walipo wahakikishiwe kwamba, wanapata elimu bora na wala si bora elimu ili kuweza kupambana na mazingira pamoja na changamoto za maisha kwa siku za usoni. Hii inatokana na ukweli kwamba, elimu ndiye mkombozi wa maskini!

Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Mama Kanisa anaendelea kukazia umuhimu wa malezi bora kwa vijana katika medani mbali mbali za maisha, ili waweze kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Mikakati ya malezi ya vijana ipewe msukumo wa pekee katika ngazi mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa.

Vijana wakifundwa barabara na kuwa ni Wakristo wema, hapana shaka kwamba, watakuwa pia ni raia wema watakaojenga na kuimarisha misingi bora ya kifamilia, hapa familia zitakuwa ni viota vya miito mbali mbali ndani ya Kanisa. Malezi bora na makini ni ujenzi wa Jamii bora kwa sasa na kwa siku za usoni.

Sr. Maria Eugenia Thomas anasema, vijana wasaidiwe kuwa ni watu kadiri ya mpango wa Mungu. Jamii na Kanisa ni wadau wakubwa katika ujenzi wa vijana wa kizazi kipya katika medani mbali mbali za maisha. Elimu na malezi bora yapewe msukumo wa pekee katika maisha ya vijana.







All the contents on this site are copyrighted ©.