2013-08-10 10:11:44

Papa atembelea maeneo ya Viwanda mjini Vatican


Wafanyakazi wa maeneo ya viwanda mjini Vatican, walishikwa na butwaa pale Baba Mtakatifu Francisko alipowatembelea kwenye maeneo yao ya kazi mapema siku ya Ijumaa, tarehe 9 Agosti 2013. Wafanyikazi waliobahatika kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu ni: Waseremala, mafundi bomba, mafundi umeme na baadhi ya waandishi wa habari wa Gazeti la L’Osservatore Romano waliokuwa wanachungulia kutoka kwenye ofisi zao.
Mshtuko wa furaha uliwakumba wafanyakazi hao kwani hawakuwa wanamtarajia Baba Mtakatifu kuwatembelea katika maeneo ya kazi. Mmoja wa wafanyakazi hao ameiambia Radio Vatican kwamba walishangaa kuona gari la Baba Mtakatifu kwenye maeneo hayo na kwamba kwa miaka kumi aliyofanya kazi mjini humo, tukio kama hilo halijawahi kutokea.
Kila kuchapo Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwashangaza wengi kwa namna yake ya kuwajali watu wa tabaka zote na kuonyesha mshikamano nao kwa kuwakaribia kwa mapendo. Tukio la kuwatembelea wafanyakazi hawa wa Vatican limeacha chapa kubwa kwenye maisha yao.
Wanasema, licha ya kuwa na fursa ya kumwona na kushiriki na Baba Mtakatifu Francisko Kanisani wakati wa ibada ya Misa huko Domus Sanctae Martha, walijihisi tofauti sana kumwona na kuongea naye kwa karibu zaidi na hasa kwenye maeneo yao ya kazi; hii ndiyo ari na roho ya uinjilishaji mpya inayopania kutolea ushuhuda wa Kristo na Kanisa lake katika medani mbali mbali za maisha.
All the contents on this site are copyrighted ©.