2013-08-10 08:06:25

Nia za Papa kwa Mwezi Agosti, 2013


Nia ya jumla ya Baba Mtakatifu katika Mwezi Agosti 2013 ni ili kwamba wazazi na walezi waweze kuwasaidia vijana wa kizazi kipya kuwa na dhamiri nyofu pamoja na maisha. RealAudioMP3

Elimu ya haki na amani kwa vijana wa kizazi kipya, ndiyo kauli mbiu iliyoongoza Maadhimisho ya Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2011, ili kuwasaidia vijana waweze kuchangia ari, mwamko na mawazo katika mchakato wa kuleta matumaini mapya duniani.

Ni ujumbe ambao uliwalenga wadau mbali mbali katika masuala ya elimu kwa vijana wa kizazi kipya, akiwataka kuwa makini kusikiliza na kuwapokea vijana jinsi walivyo, kwa njia ya mawasiliano chanya. Vijana wafundwe kuthamini tunu msingi za maisha na kuasha ndani mwao ari na moyo wa kujitoa kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani.

Elimu maana yake ni kuwaongoza vijana katika hija itakayowawezesha kufikia ukomavu na utimilifu wa maisha, mchakato unaotekelezwa kwa njia ya uhuru pamoja na kutambua kwamba, familia katika ulimwengu mamboleo zinakabiliwa na changamoto kibao! Kutokana na sababu mbali mbali, wazazi na walezi wanajikuta wakati mwingine hawana nafasi kwa ajili ya malezi ya watoto wao.

Hali hii inatia uchungu na kuwanyima watoto haki msingi ya kuweza kurithi: mang’amuzi, uzoefu na tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili. Wazazi na walezi wanahamasishwa kwa njia ya ushuhuda wa mifano bora ya maisha kuwa ni chemchemi ya matumaini kwa Mwenyezi Mungu na chanzo cha haki na amani ya kweli.

Walezi kwenye taasisi za elimu ya juu ni watu wanaoheshimika na kuthaminiwa na Jamii. Ni wajibu wao kuhakikisha kwamba, kila mtu anaheshimiwa na kuthaminiwa katika utu wake, kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wawasaidie vijana kutambua miito sanjari na kukuza karama na vipaji ambavyo wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu. Elimu ilandane na dhamiri nyofu na tunu msingi za maisha ya kiroho.

Elimu iwe ni mahali pa majadiliano pamoja na ujenzi wa utamaduni wa usikivu ili kuwapokea vijana jinsi walivyo na kuwasaidia kukua na kukomaa. Vijana wajiweke tayari kusikiliza yale wanayofundishwa na walezi wao. Vijana wanahitaji kuona ushuhuda makini unaotolewa na walezi. Ikumbukwe kwamba, familia ni mahali pa kwanza ambapo mtu anaweza kujifunza misingi ya haki na amani. Familia ni kiini cha jamii na mahali ambapo tunu msingi za kiutu na kikristo zinaweza kurithishwa kwa watoto.

Hapa ni mahali pa kujifunza dhana ya mshikamano kati ya vizazi mbali mbali; mahali pa kujifunza kuheshimu na kutii sheria, toba na msamaha; mahali ambapo mtu anajisikia kupokelewa. Kimsingi familia ni shule ya kwanza ambamo watu wanajifunza haki na amani.

Nia za Kimissionari za Baba Mtakatifu kwa mwezi Agosti kwa Mwaka 2013 ni kwamba, Kanisa Barani Afrika liweze kutangaza Injili kwa uaminifu pamoja na kuhamasisha haki na amani. Hii ni changanmoto kwa Familia ya Mungu Barani Afrika kuhakikisha kwamba, inaishi mintarafu haki ya Kristo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Jamii nyingi Barani Afrika zinakabiliwa na uvunjifu wa misingi ya haki na amani.

Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika yalijadili kwa namna ya pekee: upatanisho, haki na amani mintarafu taalimungu na wajibu wa kijamii unaotekelezwa na Mama Kanisa katika medani mbali mbali za maisha Barani Afrika.

Haki na Upatanisho anasema Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita ni mihimili mikuu ya amani. Anakumbusha kwamba, amani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomwajibisha mwanadamu kujikita katika upendo. Huu ni mwaliko kwa waamini kujipatanisha na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Yesu Kristo; wawe ni mfano bora wa kuigwa katika utekelezaji wa haki na upendo.

Waamini na watu wenye mapenzi mema wanahamasishwa na Mama Kanisa kuwa ni wajenzi wa haki na Jamii inayosimikwa katika haki, kila mtu akipewa haki zake msingi. Haki inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika maisha ya hadhara na huduma mbali mbali zinazotolewa kwa wananchi Barani Afrika. Mshikamano kati ya watu wa mataifa uongozwe na kanuni auni na upendo. Ni mwaliko kwa waamini kutubu na kuongoka, daima wakiendelea kuwa ni waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake. Wanasiasa kwa upande wao wanapaswa kulinda na kudumisha misingi ya haki jamii, huku wakiongozwa na dhamiri nyofu.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita anasema kwamba, Kanisa halina majibu msingi ya kila shida na changamoto zinazojitokeza ndani ya Jamii na wala Kanisa halina lengo la kuingilia masuala ya kisiasa, lakini linayo dhamana ya kuhakikisha kwamba: haki, amani, ukweli na mafao ya wengi yanatekelezwa kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Jamii husika.

Kanisa Barani Afrika linaalikwa kuwa ni sauti ya kinabii kwa wale wote wanaoteseka na kunyanyasika kutokana na vita, kinzani na migogoro mbali mbali ya kijamii, kisiasa, kikabila na kidini. Mama Kanisa anatafuta ile zawadi ya amani ambayo Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu kwa njia ya Yesu Kristo aliyeleta upatanisho kati ya Mungu na mwanadamu na hatimaye, kulifanya Kanisa kuwa ni Sakramenti ya amani ya Mungu.
All the contents on this site are copyrighted ©.