2013-08-10 10:38:06

Juma la Maadhimisho ya Familia Brazil


Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil kuanzia tarehe 11 hadi tarehe 17 Agosti 2013 linaadhimisha Juma la Familia Kitaifa, changamoto kwa wale wanaoendelea bado kuamini na kuwekeza katika tunu msingi za maisha ya kifamilia kuendelea kusimama kidete kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia nchini Brazil.

Maaskofu wanakumbusha kwamba, Familia ni amana na urithi mkubwa ambao Amerika ya Kusini imebahatika kupata kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, hii ni hazina kwa binadamu wote. Hivi ndivyo wanavyokumbusha Mababa wa mkutano mkuu wa Aparecida. Viongozi wa Kanisa wanahamasishwa kutoa tafakari ya kina kuhusu umuhimu na tunu msingi za maisha ya familia ya binadamu kadiri ya mpango na utashi wa Mungu.

Familia zinahamasishwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuadhimisha Sakramenti za Kanisa, kufanya tafakari ya kina ya Neno la Mungu na kumwilisha ujumbe wa Habari Njema ya Wokovu katika uhalisia wa maisha yao. Kwa njia hii, familia inaendelea kutoa ushuhuda wa imani katika matendo. Ni wajibu na changamoto kwa familia pia kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi. Umuhimu wa familia unapaswa kuwagusa wote kwani hakuna mtu aliyetoka nje ya familia. Walimu na wanafunzi wapate nafasi ya kujadiliana kwa kina: kuhusu umuhimu, changamoto na fursa zilizopo kwa ajili ya familia kutekeleza wajibu wake ndani ya Kanisa na Jamii.

Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Brazil linabainisha kwamba, familia katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia inakabiliana na changamoto nyingi, jambo la msingi ni kwa wanafamilia kusimama kidete kulinda na kutetea misingi bora ya familia, maadili na utu wema. Hii inatokana na ukweli kwamba, familia ni mhimili mkuu wa maendeleo ya mtu katika medani mbali mbali za maisha.

Familia ni zawadi safi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kukuzwa na kuendelezwa na kwamba, Serikali zinawajibu wa kuzitetea na kuzilinda familia katika utekelezaji wa majukumu yake, lakini kwa bahati mbaya, wakati mwingine Serikali zimekuwa ni kinyume cha tunu msingi za kifamilia.







All the contents on this site are copyrighted ©.