Endelezeni thawabu mlizovuna wakati wa Mfungo mtukufu wa Ramadhani!
Waamini wa dini ya Kiislam nchini Tanzania wametakiwa kuutumia mfungo wa mwezi Mtukufu
wa Ramadhani ulioisha kama darasa na kuendeleza mambo mema waliyokua wakiyafanya katika
kipindi chote cha mfungo. Kauli hiyo imetolewa na Shekhe wa mkoa wa Dodoma, Mustapha
Rajabu wakati alipokuwa akihutubia waumini wa dini hiyo katika ibada ya Siku kuu ya
Id el Fitr iliyofanyika katika msikikiti wa Ghadafi kwenye Manispaa ya Dodoma.
Shekhe
Rajabu alisema kuwa Waislamu hawana budi kuutumia mwezi wa Mfungo wa Ramadhani kwao
kuwa kama semina ambayo imewawezesha kutenda mema na kuacha mabaya ambayo hayampendezi
Mungu. Alisema kwamba, haitakuwa na maana yoyote kwao kama hawatayaendeleza mambo
mazuri ambayo wamekua wakiyafanya katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Aidha ametoa
wito kwa Waislam kote nchini Tanzania kuendeleza umoja na mshikamano uliopo na kujiepusha
katika machafuko mbalimbali.
“Tuishi kwa amani na upendo na mshikamano watu
wote bila ya kujali itikadi zetu au makabila” alisema Shekhe Rajabu. Amewaonya waamini
wa dini hiyo kuacha kuitumia siku kuu hiyo kama sehemu ya kufanya maovu kupindukia
kwani ni kinyume na mafundisho ya Mwenyezi Mungu. “Tusiitumie siku hii kufanya machafuko
kama vile kulewa kupindukia bali tusherehekea siku hii kwa amani na upendo” alisema.
Naye
Shakila Nurdin, aliwaomba waumini wenzake wa dini ya kiislamu nchini waienzi amani
na mshikamano uliopo kama Mtume Mohamed (S.W.A) alivyohimiza katika vitabu vyake vitakatifu.
“Amani ikipotea tutakao pata shida ni sisi akina mama na watoto hivyo na sisi tujitahidi
kuhimiza amani kuanzia majumbani makanisani na misikitini” Alisema Shakila.
Hata
hivyo aliwaasa vijana kuepuka kukaa vijiweni bali wajishughulishe na mambo ambayo
yatawaletea maendeleo tofauti na ilivyo sasa ambapo wamekuwa wakiilaumu serikali bila
ya wao kufanya jihada zozote za kujikwamua kihali na kiuchumi.