2013-08-10 11:55:44

Balozi wa Vatican nchini Kenya aanza utume wake rasmi!


Askofu mkuu Charle s Daniel Balvo, Balozi wa Vatican nchini Kenya na Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Shirika la umoja wa Mataifa linaloshughulikia mazingira, UNEP na Shirika la Makazi ya Watu la Umoja wa Mataifa, UN habitat, ameanza utume wake kwa makaribisho makubwa yaliyoongozwa na Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya kwa niaba ya Familia ya Mungu nchini Kenya.

Akizungumza na waandishi wa habari katika tukio hili, Askofu mkuu Balvo amesema kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amemtia ari na moyo wa kutekeleza wajibu na dhamana yake mpya, kwa kutambua kwamba, anaendelea kumsindikiza kwa njia ya sala na uwepo wake wa karibu. Amepata nafasi pia ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Kanisa Katoliki nchini Kenya pamoja na wawakilishi wa Taasisi mbali mbali za Kanisa zenye makao makuu yake nchini Kenya.

Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Balvo aliwasilisha hati zake za utambulisho kwa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, hapo tarehe 28 Juni 2013. Rais Kenyatta alimhakikishia Askofu mkuu Balvo ushirikiano mkubwa kutoka katika Serikali na kwamba ni msaada mkubwa kwa Kanisa na Kenya katika ujumla wake. Askofu Balvo amewasilisha pia hati zake kwenye Mashirika ya Umoja wa Mataifa yenye makao yake makuu Jijini Nairobi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya limemwalika rasmi Askofu mkuu Charles Daniel Balvo kushiriki katika mkutano wao mkuu unaotarajiwa kufanyika Jimbo kuu la Mombasa na huo ndio utakaokuwa muda muafaka wa kuwasilisha hati zake za utambulisho kutoka kwa Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.