2013-08-10 11:34:49

Angalieni changamoto zinazojitokeza dhidi ya tunu bora za maisha ya kifamilia!


Baraza la Maaskofu Katoliki Kanda ya Ibadan nchini Nigeria linasema kwamba, Maadhimisho ya Mwaka wa Imani uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na kumbu kumbu ya Miaka 20 tangu Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili alipochapisha Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki, umekuwa ni muda muafaka ambao umeshuhudia ari na mwamko mpya katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina miongoni mwa waamini walei.

Kipindi hiki cha neema kimeshuhudia vyama vya kitume vikianzishwa na vile vya zamani vikiendelea kujipyaisha ili kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa nchini Nigeria. Waamini wengi nchini Nigeria wameboresha maisha yao ya kiroho kwa njia ya ushiriki mkamilifu wa Sakramenti za Kanisa, Tafakari ya Neno la Mungu na matendo ya huruma kwa maskini na wote wanaoteseka. Ni kipindi ambacho utume wa Biblia miongoni mwa waamini walei umepewa kipaumbele cha kwanza, ili kumfahamu, kumpenda na kumtumikia Mungu na hatimaye, kupata uzima wa milele.

Baraza la Maaskofu Katoliki kanda ya Ibadan katika mkutano wake uliofanyika hivi karibuni, limegusia hali halisi ya kisiasa na kijamii nchini Nigeria. Kwa kipindi cha miezi hivi karibuni, damu ya watu wasiokuwa na hatia imeendelea kumwagika nchini Nigeria kutokana na mashambulizi yanayofanywa na Kikundi cha Kigaidi cha Boko Haramu ambacho kimekuwa ni tishio kwa maisha na mali za wananchi wa Nigeria.

Maaskofu wanaipongeza Serikali ya Nigeria kwa hatua mbali mbali inayoendelea kuchukua ili kulinda raia na mali zao, lakini wanasikitishwa na utamaduni wa kifo unaojitokeza katika operesheni hizi, kwani watu wengi wanaendelea kupoteza maisha na kwamba, walaani kitendo cha Serikali kuanza kutekeleza adhabu ya kunyongwa hadi kufa, kwani ni kinyume cha haki msingi za binadamu.

Maaskofu Katoliki nchini Nigeria wanasikitishwa na wimbi la ongezeko la ndoa za watoto wadogo nchini humo sanjari na kuibuka kwa makundi yanayotaka ndoa za watu wa jinsia moja, jambo ambalo ni kinyume cha maadili, utu wema na utamaduni wa kiafrika. Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linaendelea kuunga mkono ndoa kati ya Bwana na Bibi kadiri ya mpango na utashi wa Mungu kwa binadamu.

Maaskofu wanawasihi waamini na wananchi kwa ujumla kuwavumilia na kuwaheshimu watu wenye hisia na mielekeo ya ushoga na wala wasitengwe, kwani hata wao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Maaskofu Katoliki Nigeria wanasema bayana kwamba, haya ni mambo ambayo kamwe wasingependa kuona yanaingizwa kwenye Katiba ya Nchi kwani ni kinyume cha maadili, utu wema na mpango wa Mungu. Ni jukumu la kila mwamini na raia mwema kuhakikisha kwamba, wanasimamia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu na utamaduni ni mila nzuri za Kiafrika.All the contents on this site are copyrighted ©.