2013-08-09 08:29:36

Vatican yapitisha sheria kupambana na utakatishaji wa fedha haramu, ufadhili wa vitendo vya kigaidi na utengenezaji wa silaha za maangamizi


Papa Francisko amepitisha sheria zinazozuia na kudhibiti utakatishaji wa fedha haramu, kufadhili vitendo vya kigaidi pamoja na utengenezaji wa silaha za maangamizi. Huu ni mwendelezo wa jitihada zilizoanzishwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kunako Desemba 2010, alipopitisha sheria zinazolenga kudhibiti vitendo vya uvunjaji wa sheria katika masuala ya fedha.

Sheria hii mpya inaonesha msimamo wa Vatican unaolenga kuzuia na kudhibiti utakatishaji wa fedha haramu, ufadhili ya vitendo vya kigaidi pamoja na utengenezaji wa silaha za maangamizi. Sheria hii inatumika kwa Vatican na taasisi zake pamoja na Mashirika na taasisi ambazo zinasimamiwa na Vatican kadiri ya sheria za Kanisa. Kwa sheria hii, Mamlaka ya Fedha na Habari mjini Vatican imeimarishwa zaidi.

Mamlaka hii itakuwa na wajibu wa kusimamia taasisi ambazo kimsingi zinajihusisha na masuala ya fedha pamoja na kutekeleza ushauri unaotolewa na Tume ya Fedha ya Baraza la Ulaya, yaani MONEYVAL na kwamba, usimamizi huu kwa sasa utatekelezwa na Mamlaka ya Fedha na Habari. Sheria hii pia inaunda Kamati ya Usalama wa Fedha ili kuratibu mchakato wa kuzuia na kudhibiti masuala ya utakatishaji wa fedha haramu, ufadhili wa vitendo vya kigaidi na utengenezaji wa silaha za maangamizi.







All the contents on this site are copyrighted ©.