2013-08-09 11:05:18

Mateso na mahangaiko ya watoto katika maeneo ya vita!


Migogoro ya kivita inaendelea kuzikumba sehemu mbalimbali za Bara la Afrika. Hivi majuzi watu zaidi ya 66,000 asilimia 55% wakiwa ni watoto wadogo wamelazimika kuikimbia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo na kutafuta usalama nchini Uganda kufuatia kuibuka kwa vita kwenye mji wa Kamango Mashariki mwa nchi hiyo, kati ya Jeshi la Mgambo Uganda ADF, na Wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo.

Taarifa ya Shirika la habari la Fides inasema kwamba vita hivyo iliibuka usiku wa manane na kuibua utata mkubwa ambapo iliwalazimu watu, hata wa familia moja kukimbilia sehemu tofauti ili kuokoa maisha yao. Katika kizaazaa hicho watoto wengi walitengana na wazazi wao na kulazimika kutemnbea umnbali mrefu kwa miguu hadi mpakani mwa Uganda ili kusalimisha maisha yao.

Hali ya maisha eneo hilo inaendelea kutia utata mwingi kwa Jumuiya ya Kimataifa, kwani ni vigumu kuweza kutoa huduma za kibinadamu. Inasemekana hadi mwezi Juni, 2013 watoto wapatao 4,500 walisajiliwa Jeshini. Na watoto 2,000 kati ya hao walitoka kwenye Jimbo la Kivu Kaskazini mwa DRC.

Mara nyingi kunapotokea vita ni wanawake, wazee na watoto wanaoathirika zaidi, changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kutafuta mbinu muafaka ya kupambana vilivyo na vita ili kudumisha amani na usalama. Inasikitisha kuona watoto wakipelekwa mstari wa mbele kama chambo wakati wa vita.. Chama cha Msalaba Mwekundu nchini Uganda kinasema, kuna watoto 37,037 ambao ni wakimbizi.








All the contents on this site are copyrighted ©.