2013-08-09 07:43:38

Mali, fedha na rasilimali ni kwa ajili ya huduma ya Watu wa Mungu na wala si mali ya mtu binafsi!


Askofu Mkuu Josephat Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha katika mahojiano na Radio Vatican anabainisha kwamba, Kanisa Katoliki linaendelea kuhimiza dhana ya ukweli, uwazi, uwajibikaji, maadili na tija kwa fedha na mali ya Kanisa. RealAudioMP3
Viongozi wa Kanisa katika ngazi mbali mbali wanapaswa kutambua kwamba, wamedhaminishwa na Mama Kanisa mali na fedha kwa ajili ya shughuli za Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitahi ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Viongozi wa Kanisa daima wajitahidi kuongozwa na dhamiri nyofu ili kuwa na matumizi sahihi ya mali na fedha ya Kanisa na kamwe wasisutwe na dhamiri nyofu mbele ya Kristo kwa kuwa na matumizi mabaya ya mali na rasilimali ya Kanisa, daima wakijitahidi kuwa waaminifu, wakweli na wawazi. Watambue kwamba, mali ya Kanisa ni kwa ajili ya mafao ya Familia ya Mungu na wala si mali ya mtu binafsi na kwamba, dhamana ya uongozi ni kwa ajili ya kuonesha dira katika hija ya Familia ya Mungu hapa duniani. Kumbe, madaraka na mali ni kwa ajili ya huduma na wala si vinginevyo!

Askofu mkuu Josephat Lebulu anasema kwamba, ili misingi hii ya maadili na uwajibikaji fungamanishi viweze kutekelezeka, kuna haja ya kuendelea kuhimiza uundwaji wa kamati za fedha na mipango kama zilivyoainishwa na Kanisa. Kamati hizi zitumike barabara kama nyenzo ya kukoleza mchakato wa maendeleo endelevu ndani ya Kanisa na kwenye taasisi, ili kukuza dhana ya uwajibikaji wa pamoja, ukweli na uwazi, tija, ufanisi na uadilifu kwa matumizi ya mali ya Kanisa.







All the contents on this site are copyrighted ©.