2013-08-09 12:02:56

Dumisheni misingi ya haki na amani kwa njia ya majadiliano!


Wawakilishi wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio nchini Tanzania, hapo tarehe 2 Agosti 2013 walijumuika kusali kwa ajili ya kuwaombea watu waliofariki dunia na wengine wengi kupata majeraha makubwa kutokana na bomu lililorushwa wakati wa ufunguzi wa Kanisa la Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti, Jimbo kuu la Arusha.

Wakati wa bomu lilipokuwa linatupwa mahali hapo, Ibada ilikuwa inaongozwa na Askofu mkuu Francisco Montecillo Padilla, Balozi wa Vatican nchini Tanzania akisaidiana na Askofu mkuu Josephat L. Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha, Tanzania. Ifuatayo ni tafakari iliyotolewa wakati wa kumbu kumbu hiyo!

Ndugu zangu kaka na dada, ni faraja kwetu kama Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, Tanzania kuwa hapa leo pamoja nanyi katika sala hii, sala ndio silaha yetu waamini ambayo hubadili mioyo na historia. Kutoka mbali au karibu tunaungana kama jamaa na marafiki. Leo kwa namna ya pekee tukiwakumbuka ndugu zetu na marafiki zetu walioathiriwa na mabomu hapa Olasiti Mwezi Mei, 2013.

Katika ubinadamu wetu ni rahisi kuwa na hasira hasa kwa jambo kama hili la mabomu yaliyotokea hapa, tuna uchungu na pengine tunatamani kisasi, lakini Yesu anatuambia wapendeni adui zenu na kuwaombea wale wanaowadhulumu nyie (Mt 5, 44) . Maisha ya wakristo wenzentu yamedhulumiwa, tumepoteza ndugu, jamaa au rafiki ila katika yote bado Neno la Mungu halibadiliki inatupasa kusamehe na kuonyesha upendo. Yesu anataka tupingane na dhana ya kisasi.

Kama tukilipiza ubaya kwa ubaya hatutatatua tatizo, bali tutazidi kulichochea. Yesu anatupa njia mbadala ya kupambana na uovu na ni kwa njia ya upendo. Hatuwezi kushinda uovu kwa uovu, bali kwa wema. Yesu ametuonyesha hayo kwa mifano, Yesu anasema, mmesikia imenenwa mpende jirani yako na mchukie adui yako, lakini mimi nawaambia mpende adui yako. Yesu anafuta uadui na kutuamuru upendo maana kwake hakuna adui na sote ni majirani.

Injili inatutaka sisi tusamehe kila jambo. Ni ngumu hasa tunapokuwa tumeumizwa na kuonewa, lakini pia Yesu anatuambia tuwaombee wanaotudhulumu kama Yeye alivyofanya pale Msalabani aliposema Baba uwasamehe kwa vile hawajui watendalo (Lk 23, 34).

Ndugu zangu, ndio maana tuko hapa leo kumwomba Mungu kwa alili ya walioathirika, kwa ajili yetu na hasa kwa ajili ya wale waliosababisha madhara haya. Tuko hapa kumwambia Mungu awasamehe wote waliohusika na mabomu hapa kwetu, kwa maana hawakujua watendalo. Huu ni wakati wa kuithibitisha imani yetu na ukristo wetu kwa kuifuata Injili hata kama katika ubinadmu wetu ni vigumu.

Ndugu zangu Injili imetuambia wazi hakuna faida katika kuwapenda tu wanaotupenda maana hata watoza ushuru na wanyang’anyi hufanya hivyo, upendo wetu hautakiwi uwe na mipaka. Upendo hauhesabu mabaya, hivyo wote tumeitwa kuwa wakamilifu kama Baba yetu alivyo mkamilifu. Tukianza kwa kuwasamehe wale waliosababisa mabomu hapa kwetu Olasiti na kuwaombea. Lakini pia kutafuta suluhisho na upatanisho kwa njia ya mazungumzo ya amani.

Majadiliano ya kidinii na Kiekumene na madhehebu mbali mbali ni muhimu ili kwa pamoja tuangalie namna tunavyoweza kufikia amani. Mazungumzo hayamwondolei mtu yeyote utambulisho wake, bali humwezesha mtu kugundua uzuri wake na kuona uzuri wa wengine. Jamii yetu inabidi ijifunze tena namna ya kuishi pamoja.

Neno la Mungu linatutoa katika tabia za utofauti, linaondoa uchungu na pia linatupa majibu. Na sisi kama Wakristo jibu letu ni ‘amani’. Huu ni wakati wa kufikiria tena uhitaji wa kukaa na kujadiliana na mikutano na watu wa dini na madhehebu tofauti namna ya kujenga na kudumisha utamaduni wa amani. Mara nyingi watu hutumia dini kama chanzo cha mifarakano, na sisi hapa Olasiti ni mashahidi wa hili lakini dini yoyote ni chanzo cha kweli cha amani katika jamii. Katika utamaduni na undani wa kila dini neno ‘amani’ limesisitizwa. Kuwa watu wa dini kunatufundisha kuwa watu ambao tunafundisha upendo na namna ya kuishi pamoja. Sote tuelewe kwamba tupo hapa kwa ajili ya upatanisho,

Tunaamini pia tunaweza kuendeleza urithi huu wa amani ambao tulipokea toka kwa Baba wa Taifa, Mwalim Julius Kambarage Nyerere. Tanzania tupo katika hatari ya kusahau urithi wetu. Inabidi tuurudie, tuuishi na tuusambaze pia kwa kizazi kipya na kijacho. Tuishi maisha yetu na azimio la kuwa wajenzi wa amani. Kila mmoja wetu anatakiwa awe ni uwepo wa amani, upatanisho na sala.

Tunahitaji kuongea juu ya amani na tunahitaji watu wa amani ili yaliyotokea hapa Olasiti na yasitokee kwingineko. Uwepo wa amani usibague dini wala dhehebu. Katika nchi ambayo tuko katika hatari ya kusahau misingi ya kuishi pamoja ambayo tumejengewa.

Ndugu zangu, leo tunatiwa nguvu kuendelea na moyo wa amani na upendo hata katika wakati huu mgumu, ili kuubadili. Na pia tuendelee kuomba kwa nguvu. Sala zetu zitengeneze mazingira mapya yanayotunzunguka. Na kutulinda sisi sote tuweze kushinda nguvu za uovu.

Wapendwa, tuziombee roho za ndugu zetu waliopoteza maisha pumziko la milele mbinguni. Familia na marafiki, Mungu azidi kuwatia nguvu na faraja na zaidi moyo wa msamaha. Kwa ajili ya nchi yetu na kanisa letu lote. Tuanze upya na kwa nguvu za roho mtakatifu kutengeneza wakati wa tumaini kwa Olasiti, Tanzania na dunia nzima.








All the contents on this site are copyrighted ©.