Baba Mtakatifu awapongeza wanachama wa Knights of Columbus kwa mshikamano wa dhati
na maskini!
Chama cha kitume cha "Knights of Columbus", kimehitimisha mkutano wake mkuu wa 131,
uliofunguliwa hapo tarehe 6 hadi 8 Agosti 2013 huko San Antonio Texas, Marekani. Hiki
ni chama ambacho kimekuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia watu wanaosukumizwa pembezoni
mwa Jamii mintarafu imani na mshikamano wa kidugu ndani ya Kanisa.
Ni chama
ambacho kimelisaidia Kanisa Katoliki katika utekelezaji wa mikakati ya shughuli za
kimissionari sehemu mbali mbali za duniani. Huu ni ushuhuda wa imani tendaji unaojionesha
miongoni mwa wanachama wa chama hiki.
Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu
Francisko kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa Chama cha Kitume cha "Knights of Columbus"
ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Tarcisio Bertone, katibu mkuu wa Vatican.
Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza kwa kumwilisha imani katika maisha ya hadhara
na hivyo kuwawezesha waamini kushiriki kikamilifu utume wa Kanisa katika ngazi mbali
mbali. Hiki ni chama kinachoonesha kwa mapana uhuru wa kuabudu, ambao ni haki msingi
inayoonesha ukomavu wa kidemokrasia katika nchi yoyote ile.
Baba Mtakatifu
Francisko anawataka wanachama hao kurithisha tunu msingi za maisha ya kifamilia kwa
kuzingatia udumifu na uaminifu kwa ajili ya kizazi kipya; utu na heshima ya binadamu;
haki na usawa pamoja na kulisaidia Kanisa kutekeleza dhamana na utume wake ulimwenguni.
Anawataka wawe mstari wa mbele katika kulinda na kutunza mazingira.
Ushuhuda
makini kwa Kristo na Kanisa lake, unajikita kwanza kabisa katika toba na wongofu wa
ndani; kwa kusimama kidete kulinda tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kadiri
ya mpango wa Mungu kwa mwanadamu. Kama wanachama watambue utakatifu wa maisha na tendo
la ndoa kadiri ya mpango wa Mungu. Waamini wanaalikwa kutembea katika mwanga wa imani
kwa kuonesha maana ya maisha, kwa kujenga na kudumisha mshikamano wa kidugu na mapendo;
wakihudumia na kujenga Jamii inayosimikwa katika utu na heshima ya binadamu.
Takwimu
zinaonesha kwamba, idadi ya wananchama imeongezeka maradufu na kwa sasa kuna wanachama
1,843,587. Washauri wameongezeka hadi kufikia watu 14,606. Chama hiki kina wachama
wengi zaidi nchini Lituania, Ucrain na Poland. Jumla ya dolla millioni 167 zimetumika
kwa ajili ya maskini na wahitaji zaidi. Chama hiki kinaendelea kuwagusa watu kutoka
katika undani wa maisha yao kwa njia ya huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii.
Huu ni ushuhuda wa huduma ya upendo inayotekelezwa kwa
moyo wa ukarimu na mshikamano wa dhati, changamoto endelevu inayohimizwa na Baba Mtakatifu
Francisko kwa Kanisa na watu wenye mapenzi mema. Waamini wanahamaishwa kushiriki kikamilifu
katika azma ya Uinjilishaji mpya kwa hali na mali, kama alivyokazia Kardinali Sean
Patrick O'Malley wa Jimbo kuu la Boston, nchini Marekani.