Papa Francisko atuma salam za rambi rambi nchini Argentina
Baba Mtakatifu Francisko amemtumia salam za rambi rambi Askofu mkuu Josè Luis Mollaghan
wa Jimbo kuu la Rosario, lililoko nchini Argentina kutokana na kuporomoka kwa jengo
ambalo limesababisha watu 12 kufariki dunia, wengine 60 kujeruhiwa vibaya na 16 hadi
sasa hawajulikani waliko. Jengo hili limeporomoka baada ya kuvuja kwa gesi mapema
juma hili.
Ujumbe wa Baba Mtakatifu umeandikwa kwa niaba yake na Kardinali
Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican. Baba Mtakatifu Francisko anaonesha masikitiko
na uchungu mkubwa na anapenda kuungana na wote wanaoomboleza msiba huu mkubwa kwa
njia ya sala na sadaka yake. Anawaombea majeruhi ili waweze kupona haraka na kuendelea
na shughuli zao za kila siku. Ujumbe huu wa Baba Mtakatifu umesomwa wakati wa Maandamano
ya Maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Gaetano, Msimamizi wa Argentina, hapo siku
ya Jumatano, tarehe 7 Agosti 2013.