Karibu ndugu msikilizaji katika hema la vijana ndani ya studio za Radio Vatican Baada
ya maadhimisho ya 28 ya siku ya vijana duniani, nahisi msukumo ndani ya moyo kushirikishana
nawe au kukumbushana machahche ya muhimu yaliyojili Rio de Janeiro. Hii ni kwa sababu
ya jinsi alivyotugusa Baba Mtakatifu Fransisko kwa upendo mkubwa, na sababu ya upendo
nilio nao kwako. Natumaini wote mliokuwa Rio de Janeiro, Brazil mtakuwa mmekwishafika
nyumbani. Pole sana kwa safari na uchovu, na hongereni kwa kukamilisha hija hiyo ya
imani na matumaini. Naamini matunda mengi ya: Imani na Sakramenti; Marafiki na hata
ya uchumba yatajionesha kwa wakati muafaka. Mimi nawaombea kila jema katika hija ya
maisha ya ujana! Nendeni ulimwenguni kote mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi
wangu (Mathayo 28, 19). Maneno hayo ya Bwana Yesu kutoka Injili ya Mathayo, ndiyo
yalikuwa mada, au kauli mbiu ya maadhimisho haya ya 28 ya vijana kimataifa. Tunapokwenda
kuwafanya watu kuwa wanafunzi katika familia zetu, sehemu za kazi, mashuleni, na katika
jamii kwa ujumla, kuna mambo yaliyogusa sana maadhimisho ya vijana na maneno ambayo
Baba Mtakatifu Francisko kasisitiza. Wakati wa Ibada ya Njia ya Msalaba Baba Mtakatifu
Francisko katualika tuchukue maisha yetu na kila kitu tulichonacho tumpelekee Yesu
Msalabani. Furaha yetu, taabu na mahangaiko yetu, mafanikio na kushindwa kwetu. Twende
kwa Yesu yeye ambaye ametuamini na kutupa utume huu wa kutangaza Injili yake. Tarehe
23 Julai, Siku ya kwanza tu alipowasili Rio, alisema kuwa Kristu katuamini vijana
ndio sababu katukabidhi utume huu wa kuishuhudia Injili. Na ni matumaini yake Baba
Mtakatifu Fransisko kuwa sisi vijana pia hatuogopi kumkabidhi Kristu maisha yetu.
Ujumbe huu unatukumbusha maneno ya Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa kumi na
sita, katika Misa yake ya kwanza ya utume wake kama khalifa wa Petro mnamo mwaka 2005,
alisema: vijana msiogope kumwamini kristu kwani hachukui uhuru wenu wala chochote
kutoka kwenu, badala yake anawapa kila kitu. Katika madhabahu ya Bikira Maria wa
Aparecida Baba Mtakatifu Francisko kakusisitiza kijana udumu katika matumaini, ujiachie
na kuruhusu kushangazwa na Mungu sababu Mungu wetu ni Mungu wa ma suprise kwani amesheheni
upendo na maajabu kemkem, pia kakusisitiza uishi kwa furaha, kwani ndivyo Mwenyezi
kanuia tangu mwanzo wa uhai wetu, tuishi kwa furaha. Weka bidii katika michezo
na uchukue michezo kama sehemu ya kukua kimwili na kiroho na sio kujenga uadui na
ugomvi kati ya watu. Kumbe, wakati wa michezo tuburudike na tujenge urafiki zaidi. Alipotembelea
Hospitali ya Mt. Francisko wa Assis aliwafariji wagonjwa wa afya ya akili na hasa
wale walioathiriwa na dawa ya kulevya. Baba Mtakatifu Fransisko amelaani vikali matumizi
haramu ya dawa za kulevya na anawaalika wote wanaofanya biashara hii kuacha ili kuepuka
kuharibu maisha ya vijana. Zaidi Baba Mtakatifu Francisko kakualika kuwaheshimu
na kuwasikiliza wazee. Mwaliko huu kausisitiza kwa namna ya pekee, katika maadhimisho
ya kumbukumbu ya watakatifu Yoakimu na Anna, babu na bibi wa Bikira Maria. Nuru hii
tulioipokea pamoja na mema mengi yaliyojiri Rio de Jeneiro, tuipeleke ulimwenguni
kote tulipo. Napenda kukukumbusha pia kuwa maadhimisho yajayo ya siku ya 29 ya
vijana kimataifa yatafanyikia Cracovia, Poland mnamo mwaka 2016, yaani miaka mitatu
kuanzia sasa. Kumbe, anza maandalizi mapema ili uweze kushiriki maadhimisho hayo. Sina
la ziada, endelea kumshuhudia Kristo kwa maneno na matendo pamoja na kuendelea kuwafanya
wengi kuwa wanafunzi wake. Mpaka kipindi kingine tena. Kutoka Studio za Radio Vatican,
ni mimi mtumishi wa Altare ya Bwana, Padre Celestin Nyanda.