2013-08-08 09:59:32

Maadhimisho ya Siku ya 47 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni na changamoto zake nchini Tanzania


Mama Kanisa daima ameendelea kusoma alama za nyakati katika dhamana na utume wake wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Kama ilivyokuwa kwa Mitume na Wafuasi wa Yesu wakati ule wa Kanisa la mwanzo, walijitosa kimasomaso bila kuogopa vikwazo na vipingamizi ambavyo wangeweza kukutana navyo katika utekelezaji wa utume wao kwa watu wa mataifa.

Katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, Kanisa limejikuta linakabiliana na changamoto ya utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Huu ni ulimwengu mpya ambao unapaswa kumfahamu na kumtambua Mwenyezi Mungu, ili watu wengi waweze kufaidika na maendeleo haya ambayo kimsingi ni utajiri mkubwa wa binadamu.
Ujumbe wa Baba Mtakatifu mstaafu katika Maadhimisho ya Siku ya 47 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni unaongozwa na kauli mbiu “Mitandao ya Kijamii ni milango ya ukweli na imani, fursa mpya za Uinjilishaji”. Hii inaonesha dhamira ya Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika matumizi sahihi ya mitandao ya Kijamii kama milango ya ukweli na imani; haya ni majukwaa mapya yanayoundwa na mitandao hii, ili kuweza kukutana na umati mkubwa wa vijana wa kizazi kipya ambao wana kiu na njaa ya kusikia Neno la Mungu.
Kuna haja kwa Mama Kanisa kuwafuata huko huko kwenye mitandao ya Kijamii, kama alivyofanya Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita na mwendelezo huo tunauona kwa Papa Francisko kwa wakati huu katika ukurasa wake wa twitter.
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, limeadhimisha Siku ya 47 ya Upashanaji habari Ulimwenguni, hapo tarehe 4 Agosti 2013. Askofu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki Dodoma, akihojiana na Radio Mwangaza FM, amewataka viongozi waliokabidhiwa madaraka na umma kuwa makini na kauli wanazozitoa, ili kuepuka uchochezi unaoweza kupelekea kuvunjika kwa misingi ya haki, amani na utulivu. Amewataka watanzania kujenga utamaduni wa kutumia mitandao ya kijamii ili: kujifunza, kupata habari, kurithisha tunu msingi za kiroho, kimaadili na kiutu pamoja na kuburudika.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, alijitwalia dhamana ya kuhakikisha kwamba, anajitahidi kuwapo kwenye maskani ya watu, ili kuweza kuzima kiu na njaa ya watu hawa katika kumtafuta, kumfahamu, kumpenda na kumtumikia Mwenyezi Mungu. Inaweza kuonekana kwamba, ni juhudi kidogo, lakini haya ni matone ya ukweli na upendo yanayomsindikiza mwanadamu katika hija yake ya maisha na mapambano yake katika jangwa la utupu na kinzani za maisha.
Askofu Nyaisonga anaendelea kuwahimiza watanzania kutumia fursa mbali mbali za maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari ili kukuza na ujuzi na ufahamu wao. Watumie fursa zinazotolewa na mitandao ya kijamii, ili kujenga urafiki pamoja na kukutana na watu mbali mbali, lakini daima wakiwa makini na matumizi sahihi ya mitandao hii.
Hii inatokana na ukweli kwamba, baadhi ya habari na ujumbe unaotolewa kwenye mitandao hii umekuwa na mwelekeo potofu, isiyozingatia maadili na utu wema; ni ujumbe ambao wakati mwingine unachochea chuki na uhasama katika jamii, mambo hatari kwa ustawi na maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Wainjilishaji wanapaswa kusoma alama za nyakati na kutambua kwamba, wanatumwa kutangaza Injili ya Kristo kwanza kabisa kwa Jamii inayowazunguka sanjari na kutumia fursa mbali mbali zinazoendelea kuibuliwa na ulimwengu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari, kwa kupanua wigo na idadi ya walengwa katika huduma hii, lakini jambo la msingi ni majiundo makini kwa Wainjilishaji hawa! Ujumbe unaotangazwa unajikita kwa Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu! Huu ndio ujumbe unaopaswa kugusa mioyo, akili na maisha ya watu wa nyakati hizi.
Matumizi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari ni changamoto iliyotolewa kwanza kabisa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, leo hii Vatican ni kati ya taasisi zenye mitandao mikubwa inayobeba watumiaji wengi na watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwa nia ya kuwasiliana pamoja na kulifahamu Kanisa. Kwa njia ya za mitandao ya kijamii, watu wengi wanapata fursa ya kufahamu ujumbe wa Baba Mtakatifu, vinginevyo wangeendelea kubaki katika giza.










All the contents on this site are copyrighted ©.