2013-08-08 10:25:31

Jengeni mshikamano wa upendo na maskini kwa njia ya Sala, Tafakari, Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa pamoja na Matendo ya huruma!


Tunautumainia msaada wako ndiyo kauli mbiu inayoongoza siku ya mshikamano kitaifa nchini Argentina, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 8 Septemba, Siku ambayo Mama Kanisa pia anafanya kumbu kumbu ya kuzaliwa kwa Bikira Maria.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican, anawatakia kila la kheri na baraka, waamini na wananchi wote wa Argentina watakaoshiriki katika maadhimisho hayo. Baba Mtakatifu anaendelea kuwahamasisha na kuwahimiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini Argentina kukuza na kudumisha moyo wa mshikamano wa upendo unaobubujika kutoka katika imani ambayo Mwenyezi Mungu amewakirimia waja wake.

Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kabisa kujitambulisha na Kristo kwa kuendelea kujenga na kudumisha urafiki kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na Matendo ya huruma. Kwa njia hii wataweza kupata nguvu za kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kutokana na hali yao ya maisha.

Mwaka jana, kiasi cha dolla za kimarekani millioni 2.9 zilipatikana kutokana na mshikamano huo. Fedha hizi zimegharimia miradi mbali mbali ya Kanisa Katoliki nchini Argentina katika mchakato wa kupambana na umaskini wa hali na kipato.







All the contents on this site are copyrighted ©.