Viongozi mbalimbali wa kidini siku ya Jumatano, tarehe 7 Agosti 2013 waliongoza Ibada
ya sala mbele ya Hospitali ambapo amekuwa akiuguzwa kwa miezi miwili sasa aliyekuwa
Rais wa Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela. Askofu mkuu Joe Seoka wa Jimbo kuu
la Preitoria, Kanisa Anglikani alitumia muda huo kuwaomba wananchi wa Afrika Kusini
kuendelea kumuombea Mzee Mandela ambaye amekuwa akitibiwa ugonjwa wa mapafu tangu
tarehe 8 Juni, 2013, kwenye Hospitali ya Mediclinic iliyoko mjini Pretoria. Kwa
miezi hii miwili Afrika Kusini, familia, ndugu, jamaa na marafiki pamoja na watu wenye
mapenzi mema duniani kote, wamekuwa wakimwombea na kumpelekea salamu za matashi mema
Mzee Madiba, aliyewahi kupata tuzo ya amani duniani. Askofu mkuu Seoka anasema
kwamba Mwenyezi Mungu anamtumia “Mzee Madiba” na ugonjwa wake kama changamoto kwa
wananchi wote wa Afrika Kusini kuweza kuungana na kuyashikilia maadili ambayo aliyapigania
Rais huyo wa zamani. Nelson Mandela alitimiza miaka 95 akiwa hospitalini humo tarehe
18 Julai 2013.