2013-08-07 09:05:13

Uhakika wa usalama wa chakula unapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza!


Jumuiya ya Kimataifa inapoendelea kukabiliana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa pamoja na mabadiliko ya tabia nchi, kuna haja kwa wadau wa sekta ya kilimo kuhakikisha kwamba, wanatoa kipaumbele cha kwanza katika uzalishaji wa chakula ili Jumuiya ya Kimataifa iweze kuwa na uhakika wa usalama wa chakula. RealAudioMP3

Juhudi hizi zinapaswa pia kuelekezwa katika mchakato wa upandaji na utunzaji wa misitu pamoja na uvuvi bora, kwa lengo la kutaka kuwa na uhakika wa usalama wa chakula, jambo ambalo ni nyeti kwa wakati huu kutokana na idadi idadi kubwa ya watu kuendelea kuteseka kutokana na baa la njaa duniani.

Mikakati ya Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO zinaonesha kwamba, nchi wanachama zimeendelea kutoa kipaumbele cha kwanza katika sekta ya kilimo, kama njia ya kuchochea maendeleo ya mwanadamu sanjari na kuongeza tija na uzalishaji katika sekta ya kilimo.

Ni mchango uliotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Luigi Travaglino, Mwakilishi wa Vatican kwenye Mashirika ya Chakula na Kilimo ya Umoja wa Mataifa mjini Roma. Ni matumaini ya Vatican kwamba, katika kipindi kijacho, msukumo zaidi utaendelea kutolewa kwa wadau wa sekta ya kilimo kuwekeza zaidi katika shughuli za uzalishaji zinazotekelezwa na wakulima wadogo wadogo, kama njia ya kupambana na umaskini unaowakabili wananchi wengi wanaoishi vijijini, ili kuweza kupatambana na hali yao ya maisha, ili iweze kuwa bora zaidi.

Askofu mkuu Travaglino anasema kuwa Vatican inaunga mkono juhudi ambazo Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kuzifanya kwa kutoa kipaumbele kwa maboresho ya sekta ya kilimo vijijini, kwa kuwezesha familia za wakulima ili kupambana na ukosefu wa chakula na umaskini wa hali na kipato! Vatican inatambua familia kuwa ni mahali ambapo tunu msingi za kiroho, kiutu na kimaadili zinaritishwa kutoka kizazi kimoja hadi kizazi kingine.

Familia ni mahali ambapo Mapokeo hai yanatunzwa na kwamba, umefika wakati kwa wanawake ndani ya Jamii kuwezeshwa kikamilifu ili waweze kutekeleza wajibu wao katika shughuli za kilimo. Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa limeutenga Mwaka 2014 kuwa ni Mwaka wa Familia Kijijini. Kanisa Katoliki katika mikakati yake ya kichungaji limeendelea kutoa kipaumbele cha pekee kwa watu wanaoishi vijijini pamoja na kuonesha uwepo wake katika utekelezaji wa mikakati ya maendeleo vijijini.

Mwendelezo wa mfumo wa chakula unaogusa kwa namna ya pekee masuala ya teknolojia, utunzaji wa rasilimali na ubadilishanaji wa habari, hauna budi kuwashirikisha wakulima wadogo wadogo vijijini, katika kupanga na kutekeleza mikakati ya shughuli za maendeleo ya kilimo, ili kweli wakulima vijijini waweze kuchangia katika uzalishaji wa chakula cha kutosha, kikolezo cha maboresho ya hali ya maisha na maendeleo ya wakulima vijijini pamoja na kuendelea kutekeleza dhamana ya kuwa na uhakika wa chakula kwa kizazi kijacho.

Askofu mkuu Luigi Travaglino wakati akichangia kwenye mkutano wa 38 wa FAO uliohitimishwa hivi karibuni mjini Roma, anaendelea kubainisha kwamba, miongozo maalum itolewe kwa wahusika kutokana na ukosefu wa hali ya usalama wa chakula au pale ambapo kuna idadi kubwa ya watu wanaoteseka kutokana na utapiamlo na lishe bora.

Athari za myumbo wa uchumi kimataifa, zisiifanye Jumuiya ya Kimataifa kushindwa kuangalia vipaumbele vingine katika kupanda na kuhifadhi misitu, uvuvi na biashara katika sekta ya kilimo. Majadiliano ya wadau mbali mbali yajadili na kulenga mambo msingi yanayopania kuwa na uhakika wa usalama wa chakula na wala si kwa ajili ya wajanja wachache kujipatia utajiri na faida kubwa! Bei kubwa ya mazao ya chakula yana athari kubwa kwa wengi, lakini kwa namna ya pekee kwa watu wanaoishi katika Nchi changa zaidi duniani.

Wakulima katika nchi zinazoendelea wanapaswa kusaidiwa ili kuzalisha chakula cha kutosha na ziada kuiuza kwenye soko la kimataifa. Yote haya anasema Askofu mkuu Luigi Tragavaglino, Mwakilishi wa Vatican kwenye Mashirika ya Kilimo na Chakula yanapasa kuzingatia kanuni maadili; mshikamano unaoongozwa na kanuni auni katika kupanga na kutekeleza mikakati hii, ili Jumuiya ya Kimataifa iweze kufurahia amani na utulivu!
All the contents on this site are copyrighted ©.