2013-08-07 11:47:49

Kanisa Katoliki nchini Madagascar lakanusha taarifa kwamba, CRS inatoa dawa za kuzuia na kudhibiti mimba kinyume cha mafundisho ya Kanisa Katoliki!


Askofu Mkuu Odon Razanakolona wa Jimbo kuu la Antananarivo, Madagascar, amekanusha madai kwamba Shirika la Misaada la Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, CRS lilihusika kwenye ugavi wa dawa za kukinga na kutoa mimba nchini Madagascar.

Askofu Mkuu Razanakolana aliyasema hayo alipokuwa akizungumza kwenye simu na askofu Gerald Kicanas, mwenyekiti wa bodi ya CRS pamoja na wajumbe wengine wa CRS na Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani.

Askofu mkuu Razanakolona ni kiongozi wa pili wa Kanisa katika kipindi cha siku chache kukanusha madai hayo yaliyochapishwa hivi karibuni na Taasisi ya Kimataifa cha Utafiti wa Idadi ya watu. Askofu mkuu Razanakolona anasema, alishangazwa na kuona akinukuliwa kwenye ripoti ya utafiti wa Taasisi na kwamba ana uhakika kabisa CRS hufuata Mafundisho ya Kanisa na haijajishughulisha na ugawaji wa dawa za kukinga na kutoa mimba.

Hivi karibuni, Askofu Mkuu Desire Tsarahazana wa Jimbo kuu la Toamasina, ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Madagascar alionyesha mshikamano wake na shirika la CRS huku akisema kwamba, kwenye jimbo lake, CRS huendesha shughuli zake kulingana na Mafundisho Jamii ya Kanisa Katoliki.

Ripoti ya uchunguzi wa shughuli za shirika la CRS nchini Madagascar iliyochapishwa na Taasisi ya Utafiti wa idadi ya watu duniani, inadai kwamba, Shirika hilo, linaloendeshwa na misaada kutoka Kanisa Katoliki Marekani, lilikuwa linagawa dawa za kuzuia na kutoa mimba, kinyume cha Mafundisho na msimamo wa Kanisa. Hata hivyo, madai haya sasa yamekanushwa na Kanisa Katoliki nchini Madagascar.








All the contents on this site are copyrighted ©.