2013-08-07 10:20:33

Amani ya kweli inawakumbatia wote!


Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani katika hija yake ya kichungaji nchini Japan, tarehe 7 Agosti ameshiriki katika chakula kilichoandaliwa na Taasisi ya Nagasaki kwa ajili ya majadiliano ya kidini ili kudumisha amani duniani, kama sehemu ya kumbukumbu ya miaka 68 tangu Nagasaki iliposhambuliwa kwa bomu la atomic.

Kardinanli Turkson anasema tarehe 9 Agosti 1945, bomu la pili lilitupwa mjini Nagasaki, likaacha maafa makubwa katika maisha ya wananchi wengi wa Japan na ulimwengu kwa ujumla. Anasema, uwepo wake mjini Nagasaki ni hija ya kukumbuka wale waliopoteza maisha yao kutokana na Vita kuu ya Pili ya Dunia. Kwa pamoja kama wawakilishi wa dini na madhehebu mbali mbali wanafanya hija kwa ajili ya kukumbuka maafa yaliowapata wananchi wa Japan.

Kanisa Katoliki linafundisha kwamba, Mwenyezi Mungu alimuumba mwanadamu ili aweze kuwa na maisha, uhuru na furaha ya kweli, lakini kwa bahati mbaya mateso na mahangaiko yanaendelea kumwandama mwanadamu katika hija ya maisha yake hapa duniani. Maendeleo ya mwanadamu hayana budi kujisimika katika msingi wa haki na amani sanjari na kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu.

Mama Kanisa anaendelea kuadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 50 tangu Mwenyeheri Yohane XXIII alipochapisha Waraka wa kichungaji, Pacem in Terris, Amani Duniani, changamoto ya kuendelea kutambua kwamba, amani ni tunu inayowakumbatia wote na wala haimtengi mtu! Kila mtu anapaswa kuwa ni chombo na mdau wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na utulivu duniani.All the contents on this site are copyrighted ©.