2013-08-06 11:08:48

Simameni kidete kulinda na kutetea zawadi ya maisha dhidi ya vita!


Kumbukumbu ya Miaka 68 tangu miji ya Hiroshima na Nagasaki ilipolipuliwa kwa mabomu ya atomic ni kielelezo kwamba, hata leo hii, dunia bado kuna hofu kubwa ya maafa yanayoweza kujitokeza kutokana na umilikaji wa silaha za kinyuklia. Hii ni changamoto kwanza kabisa ya kuhakikisha kwamba, watu wanasimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya maisha, ili maafa ya Hiroshima na Nagasaki yasijirudie tena duniani.

Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anasema, Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa kumi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni utakaofanyika huko Korea na ya Kusini, itakuwa ni fursa ya kuangalia tena ukakasi wa vita baridi unaoendelea kujitokeza katika Jumuiya ya Kimataifa; mataifa bado yanatishia kutumia silaha za nyuklia katika mapambano.

Dr. Tveit anasema watu wanahitaji kuishi katika amani na utulivu na wala si kuendelea kuwa na wasi wasi wa mashambulizi ya silaha za kinyuklia. Amani iwe ni jiwe la msingi katika mahusiano ya kimataifa. Wazee walionusurika kutokana na maafa ya Hiroshima na Nagasaki, wawe ni kielelezo cha matumaini ya dunia isiyokuwa na vitisho vya vita. Ni changamoto ya kulinda na kutetea zawadi ya maisha ambayo ni kwa ajili ya wote!







All the contents on this site are copyrighted ©.