2013-08-06 07:56:56

Siku kuu ya kung'ara kwa Bwana Yesu Kristo!


Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 6 Agosti anaadhimisha Siku kuu ya Kung'ara kwa Bwana. Kanisa pia linaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 35 tangu Mtumishi wa Mungu Baba Mtakatifu Paulo VI alipofariki dunia, baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na Kupokea Sakramenti za Kanisa.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, akifanya tafakari kuhusu Siku kuu hii anasema kwamba, ni muhtasari wa Mafumbo ya Kanisa, yaani Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo, ili aweze kuwaimarisha wafuasi wake katika hija ya mwanga wa imani. Ni kielelezo cha mshikamano wa dhati kati ya Kristo na kazi ya uumbaji ambayo ameikomboa kwa njia ya Msalaba.

Hii ni changamoto kwa kila mwamini kuhakikisha kwamba, anatoa nafasi kwa mwanga wa imani ili uweze kumletea mabadiliko ya dhati katika maisha, kwa kuifia dhambi na nafasi zake, ili kutoa fursa ya kuishi katika utu mpya unaofikia hatima yake katika Fumbo la Msalaba wa Kristo. Ni mchakato unaopania kumsafisha mwamini katika hija ya maisha yake ya kiroho, ili siku moja aweze kuufikia utukufu wa maisha ya uzima wa milele.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, anasema, Mtumishi wa Mungu Paulo wa sita, ni kiongozi aliyeongozwa na Msalaba wa Kristo katika maisha na utume wake. Akawa ni kielelezo makini katika kutoa maana ya uongozi kama huduma kwa ajili ya Familia ya Mungu hata katika mateso na mahangaiko ya ndani. Ni huduma iliyokuwa inaongozwa na dira na mwanga wa imani, kiasi hata cha kukubali kubeba ndani mwake shutuma ambazo hazikuwa na msingi wowote. Akapambana na tawala dhalimu katika nyakati zake, lakini daima akasimama kidete kutangaza kweli za Injili na Mapokeo ya Kanisa, huku akionesha mwanga wa imani hata katika giza la undani wa mwanadamu.

Mtumishi wa Mungu Paulo VI alikuwa ni mtu wa sala na imani thabiti; aliyekirimiwa uwezo mkubwa katika uongozi kwa njia ya diplomasia, ukomavu wa maisha ya kiroho, huku akitoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo na Kanisa lake. Alibahatika kuwa na ujasiri wa kufanya mabadiliko makubwa katika utume na maisha ya Kanisa; ujasiri ambao ulikuwa unabubujika kutoka katika imani; iliyomwezesha kufanya hija mbali mbali za kichungaji, ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani. Ni kiongozi aliyethamini majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni kwa ajili ya mafao na ustawi wa binadamu wote.







All the contents on this site are copyrighted ©.