2013-08-05 12:01:11

Waamini wanatumwa kuwa ni wahubiri wa upatanisho na amani duniani!


Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 9 Agosti 2013 anashiriki katika mchakato wa kuombea amani uliobuniwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Japan, kama sehemu ya kumbu kumbu ya waathirika wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Kardinali Turkson katika mahubiri yake anasema, Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu aligeuza Fumbo la Msalaba kuwa ni chemchemi ya amani na furaha kwa mataifa.

Yesu mfufuka alipokutana na wanafunzi wake siku ile ya kwanza ya juma na kuwasalimia, huku akiwatakia amani, wanafunzi waliondoa woga na kuanza kutoka kifua mbele kama kielelezo cha upatanisho kati yao, waliomkana na hata wakathubutu kumkimbia kwa kuogopa kipigo cha watesi wa Yesu, anawajalia nafasi ya amani na upatanisho.

Wafuasi wa Yesu wamepewa dhamana ya kutangaza pamoja na kuwa ni vyombo vya upatanisho na msamaha pamoja na kuendelea kuwaganga wote wanaoteseka kutokana na vita, ili waonje amani na utulivu wa ndani. Ikumbukwe kwamba, wafuasi wa Kristo wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia, ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Ule mwili uliosulubiwa na kuteswa, ndio uliofufuka na kupewa utukufu wa Baba. Yesu mfufuka anaendelea kubadili mateso na mahangako ya binadamu kuwa ni chemchemi ya furaha na matumaini.

Kardinali Turkson anawaalika waamini waliokuwa wamefurika kwenye Kanisa kuu la Hiroshima kwa ajili ya Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Wajapani waliofariki dunia kutokana na shambulizi la bomu ya atomiki, kutembea katika mwanga wa mafundisho ya Yesu, ili waweze kuwa kweli ni wahudumu wa upatanisho na amani. Lakini, inapaswa kukumbukwa kwamba, amani ni zawadi ambayo Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu na kila mtu anapaswa kutekeleza wajibu wake.All the contents on this site are copyrighted ©.