2013-08-05 12:02:04

Rushwa na ufisadi vinachangia kukua na kukomaa kwa makundi ya kigaidi nchini Nigeria


Kikundi cha Kigaidi cha Boko Haram ni tunda la ufisadi na rushwa nchini Nigeria. Ili kupambana vyema na kikundi hiki kuna haja ya kuziba nyufa za ufisadi ili kulinda misingi ya haki, amani na maisha ya watu. Haya yamesemwa na Askofu Oliver Dashe Doeme wa Jimbo la Maiduguri lililopo Kaskazini mwa Nigeria, alipokuwa akizungumza hivi karibuni na Shirika la Kipapa la Msaada kwa Kanisa Hitaji.

Askofu Doeme ameonesha jinsi tatizo la ufisadi lilivyoikumba Nigeria na kuvuruga uchumi unaotegemea kwa asilimia kubwa soko la nishati ya mafuta jambo ambalo lina athari nyingi kwa wananchi wa Nigeria. Sekta ya kilimo haijaweza kupata msaada wa kutosha kutoka kwa serikali, na kwamba, nchi hiyo sio kwamba ina rasilimali nyingi mno za kuweza kuutegemeza uchumi wake, hivyo kuna umuhimu wa Nigeria kuimarisha sekta mbali mbali za uchumi ili kuchangia ukuaji na ustawi wa uchumi wa Nigeria.

Majiundo makini na uwekezaji kwa vijana ni jambo ambalo linapaswa kupewa msukumo wa pekee kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Nigeria. Hii ni pamoja na kuhakikisha kwamba, vijana wanapata fursa za ajira, vinginevyo wanaweza kujikuta wametumbukizwa kwenye Kundi la Boko Haram, linaloendelea kutishia usalama wa maisha na mali za watu nchini Nigeria. Vijana wawezeshwe kiuchumi na kwa njia hii wanaweza kushinda kishawishi cha kukumbatia utamaduni wa kifo, vurugu na uhalifu.

Licha ya kuwa Nigeria imekumbwa na visa vingi vya kigaidi mara kwa mara, Askofu Doeme anawashukuru waamini wa jimbo lake kwa kuonesha ujasiri wa kiimani wanapokumbwa na changamoto hiyo. Anasema kuwa jimbo lake limeathirika sana na visa vya ushambulizi kutoka Kikundi cha Kigaidi cha Boko Haram, hata hivyo Wakristo wameendelea kutoa ushuhuda wa imani yao. Ameongezea kusema kwamba hata ujasiri wa Mapadre unawatia moyo sio tu Wakristo wa jimbo hilo, bali hata yeye pia kama Askofu.

Anasema ujasiri wa mapadre kubakia kwenye Parokia na kuendelea kutoa huduma kwa waathiriwa wa mikasa hiyo wakijua bayana wanayahatarisha hata maisha yao wenyewe, ni jambo la kutia moyo, na huenda ni kwa sababu hiyo miito mipya haipungui jimboni Maiduguri, ambapo sasa hivi kuna Waseminaristi 30 na hivi majuzi jimbo lilipata mapadri wapya wanane.

Pamoja na kuendelea kutoa huduma za kichungaji kwa ajili ya watoto yatima, wale wanaoishi katika mazingira hatarishi na wajane ambao wanaume wao wameuwawa kwenye mashambulizi ya Boko Haram. Nigeria inakabiliwa pia na changamoto ya kujenga miundo mbinu kama vile Makanisa ambayo yamechomwa moto kutokana na misimamo mikali ya kiimani, Kaskazini mwa Nigeria.








All the contents on this site are copyrighted ©.