Mchakato wa kuombea amani kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Japan
Mama Kanisa anaendelea kuadhimisha Jubilee ya miaka 50 tangu Baba Mtakatifu Yohane
wa Ishirini na tatu alipochapisha Waraka wa Amani Duniani, Pacem in Terris, ambao
umekuwa ni Waraka rejea katika kujenga, kulinda na kutetea misingi ya haki, amani
na upatanisho wa kweli miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa.
Ni waraka
ambao ulitumwa kwa watu wote wenye mapenzi mema kunako tarehe 11 Aprili 1963, wakati
ambapo dunia ilipokuwa inakabiliana na hali tete ya kuzuka kwa vita ya dunia. Hiki
ni kipindi ambacho Ujerumani ilijikuta imegawanyika na Ukuta wa Berlin uliojengwa
kunako mwaka 1961 ukawa ni kielelezo cha kinzani na mgawanyiko huu miongoni mwa wananchi
wa Ujerumani.
Marekani na Urussi zilikuwa zinapimana nguvu na uwezo wa kivita
ili kuoneshana ubabe, ambao ungeweza kugharimu maisha ya mamillioni ya watu! Cuba
nikajikuta ikibanwa na mgogoro wa makombora, ulioibuka kunako mwaka 1962, hadi leo
hii, Cuba inaendelea kugharimia mgogoro wa vita baridi na madhara yake yamekuwa ni
makubwa kwa wananchi wa Cuba kwa kipindi cha miaka hamsini kwa kuwekewa vikwazo vya
uchumi kimataifa! Kilele cha kinzani zote hizi za kivita ni pale ambapo Marekani na
Urussi zilianza kutishia kutumia silaha za kinyuklia ili kukata mzizi wa fitina! Hapa
maafa yangekuwa ni makubwa sana!
Wananchi wa Japani walionja madhara ya kinzani
na Vita kuu ya Pili ya dunia, hadi leo hii bado kuna wananchi ambao wameathirika kutokana
na mabomu ya Nyuklia yaliyorushwa nchini Japan. Kwa kutambua madhara ya vita, Baraza
la Maaskofu Katoliki Japan, limeandaa siku kumi kwa ajili ya kuombea amani, kuanzia
tarehe 6 hadi tarehe 15 Agosti, 2013.
Askofu mkuu Peter Takeo Okada wa Jimbo
kuu la Tokyo, Japan, ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Japan katika
ujumbe wake kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku kumi za Amani nchini Japan anasema kwamba,
Waraka wa Amani Duniani unatoa mafundisho ya kina juhusu haki msingi za binadamu na
wajibu wa kila mtu katika Jamii; Serikali na umuhimu wa kusimama kidete kulinda na
kutetea mafao ya wengi. Unagusa masuala nyeti ya kimataifa kama vile: ukweli, haki,
mshikamano, wakimbizi, rufuku ya matumizi ya silaha za kinyuklia pamoja na sera na
mikakati ya maendeleo endelevu yanayomgusa mtu mzima: kiroho na kimwili.
Waraka
huu unapania pamoja na mambo mengine kujenga msingi wa amani unaopata chimbuko lake
katika ukweli, haki, upendo na uhuru; mambo nyeti katika kulinda na kudumisha utu,
heshima na haki msingi za binadamu. Waraka huu unabainisha kwamba, maendeleo ya kweli
ya mwanadamu yanaweza kupatikana ikiwa kama watu wanaishi katika amani, uelewano na
mshikamano. Huu ni ujumbe endelevu hata katika ulimwengu mamboleo, ambamo, amani,
utu na heshima ya binadamu vinaendelea kukabiliana na changamoto kubwa.
Tafakari
ya kina juu ya Waraka wa Amani Duniani, sanjari na Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka
Hamsini ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, katika Mwaka wa Imani, ni fursa makini
kwa waamini kutafakari tena tunu hizi msingi katika maisha na vipaumbele vyao. Kwa
wananchi wa Japan, kuna maana ya pekee, wakati huu wanapofanya mchakato wa kutaka
kubadilisha Katiba ya Nchi ambayo kimsingi ni sheria mama!
Askofu mkuu Peter
Takeo Okada, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Japan anasema, mabadiliko ya Katiba
yanataka kuondoa vifungu muhimu sana vinavyoonesha heshima na hadhi ya binadamu mintarafu
mafundisho ya Kristo juu ya upendo na umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutetea:
maisha, utu na heshima ya binadamu.
Tarehe 28 Aprili 2013 Japan iliadhimisha
Kumbu kumbu ya Mkataba wa San Francisco, siku ile Japan ilipopewa heshima yake kama
Taifa, ingawa kuna baadhi ya wananchi wa Japan hawakutendewa haki. Tarehe 23 Juni
2013, Japan iliwakumbuka wote waliopoteza maisha yao wakati wa vita. Matukio yote
haya wanasema Maaskofu Katoliki Japan yawasidie waamini kutafakari kuhusu sera makini
za kisiasa zinazoweza kujenga na kudumisha misingi ya haki na amani.