Kumbu kumbu ya Mtaguso wa Efeso uliofanyika kunako mwaka 431
Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 4
Agosti 2013 alitambua uwepo wa makundi mbali mbali na umati mkubwa wa vijana.
Ametumia
fursa hii kuwakumbuka kwa namna ya pekee Maparoko wote kutoka sehemu mbali mbali za
dunia walipokuwa wanaadhimisha Kumbu kumbu ya Mtakatifu Yohane Maria Vianney, Msimamizi
wa Maparoko. Baba Mtakatifu anasema, anaungana nao katika sala na upendo wa shughuli
za kichungaji.
Baba Mtakatifu pia amekumbushia kuhusu Siku kuu ya Kutabarukiwa
kwa Kanisa la Bikira Maria Mkuu, lililoko mjini Roma, lililojengwa kwa heshima ya
Mama wa Mungu mara baada ya Mtaguso wa Efeso, uliofanyika kunako mwaka 431, hapo Kanisa
likamtangaza Bikira Maria kuwa ni "Theotokos" yaani Mama wa Mungu. Baba Mtakatifu
Francisko, aliwaalika waamini kusali kwa pamoja salam Maria, kwa ajili ya kumbu kumbu
ya Bikira Maria afya ya Warumi.