Familia ni shule ya kwanza ya maadili na utu wema!
Ndugu zangu wapendwa tuanze tafakari yetu ya leo kwa kuongozwa na maneno ya busara
kutoka kwa Mababa wa Mtaguso wa mkuu wa Pili wa Vatican katika tamko lao kuhusu elimu
ya Kikristo. Mababa wa Mtaguso katika kifungu namba 3 walisema “familia ni shule ya
kwanza ya fadhila za kijamii ambazo kila jamii inahitaji”. Kwa neema za Mungu
zinazopatikana katika Sakramenti ya ndoa, watoto wanaanza kujifunza kuanzia miaka
yao ya mwanzo kumpenda Mungu kulingana na imani wanayopokea katika Ubatizo, kumuabudu
Yeye, na kuwapenda jirani zao. Tunapobatizwa kila mmoja wetu anashiriki katika
kazi kuu tatu za Kristu yaani unabii kwa kumshuhudia Kristo kwa maneno na matendo
yetu; ukuhani kwa kujitoa kama sadaka kwa wenzi wetu, familia yetu na taifa zima la
Mungu; na ufalme kwa kuwaongoza wengine kwa Mungu kwa mifano bora ya maisha yetu.
Wanandoa kama viongozi wa familia wanapokea wajibu huo kwa namna ya pekee zaidi kwao
binafsi na kwa watoto wao. Ni katika familia wanandoa na watoto wanaweza kujifunza
kumcha Mungu, kutambua maana ya kupenda wanapoonja jinsi wanavyopendwa Mungu, wanavyopendana
wao kwa wao, wanavyowapenda watoto na wanavyowapenda majirani zao; watoto wanaweza
kujifunza pia maana ya msamaha jinsi wanavyoonja msamaha wa Mungu wanapomkosea, jinsi
wazazi wanavyosameheana wanapokoseana, jinsi wanavyowasameha watoto wao pale wanapokosea
na jinsi wanavyowasamehe majirani zao pale wanapowakosea. Maisha ya familia yana
mahusiano makubwa na maisha ya jamii kwa ujumla kwasababu familia inaishi ndani ya
jamii. Hivyo tunapozunguzia familia ni vyema tukapeleka fikra zetu kwenye familia
asilia ambayo ni Baba, Mama na Watoto na pili familia nzima ya Mungu ambayo inatuunganisha
sisi binadamu wote tulioumbwa kwa sura na mfano Mungu. Kama wanafamilia kwa ujumla,
tukumbuke kuwa Wahenga wetu walikuwa na maneno na misemo mingi ambayo ilikuwa na busara
nyingi katika kutoa elimu kwa jamii. Tunaposonga mbele katika ulimwengu huu wa
Sayansi na Teknolojia tutazame pia tumetoka wapi kusudi yale mazuri tusiyaache nyuma
bali tuyachukue na kusonga nayo mbele. Kwa mfano, wahenga wetu walisema, “Asiyefunzwa
na mamaye, atafunzwa na ulimwengu”. Nilipokuwa ninaitafakari methali hii, niliona
kuwa imejaa hekima nyingi ambapo ina pande tatu za msingi; kwa upande mmoja inalalenga
jukumu la wazazi katika kutoa malezi bora kwa watoto; upande mwingine watoto kuwatii
na kuwaheshimu wazazi kwani wakiwa wakaidi ulimwengu utawafanza; na upande wa tatu
ni ulimwengu lakini mpaka pale tunapouchia ulimwengu utoe malezi ya msingi kwa mtoto
tayari tunakuwa tumeruka hatua muhimu ya malezi ambayo yalitakiwa yafanyike katika
ngazi ya familia. Pia tuendelee kukumbuka busara za wahenga wetu kuwa “uchungu
wa mwana aujuaye mzazi”. Malezi ambayo tutauchia ulimwengu umpatie mtoto, hayawezi
kuwa sawasawa na malezi ya wazazi. Zaidi ya elimu inayopatika katika familia,
inatupasa tukumbuke kuwa wana familia nzima ya Mungu tunawajibika katika kutoa mifano
bora kwa watu wanaotuzunguka kwa lengo ya kujenga familia na jumuiya zenye mapendo,
haki na amani . Tukijaribu kutafakari maisha yetu ya ya kifamilia na kijamii tutakuja
kugundua kuna mambo mengi yanayotokea. Mengine ni mambo mazuri na mengine hayapendezi
kwasababu hayadhihirishi upendo kwa nafsi zetu wenyewe, kwa Mungu na kwa jirani zetu.
Mara nyingi sisi binadamu, mambo yanapokwenda vizuri katika mazingira Fulani tunafurahia
na pia tunapenda hata kushiriki katika kujipatia sifa, lakini mambo yanapokwenda vibaya
tunatafuta sehemu ya kutupia lawama na sisi kujiweka pembeni kama kwamba hatuhusiki
kabisa. Katika matukio mbali mbali mbali yanayotokea, ninawaomba leo hii tujaribu
kutafakari heshima ya utu katika familia zetu tukitazama mauaji ya Albino wasiokuwa
na hatia yoyote kutokana na imani za kishirikina na ulafi wa mali ambazo tukifa tunaviacha
vyote! Ni watu wangapi wanao uwawa kutokana utoaji mimba na mauaji ya bidanamu
wenzetu wengi wasiokuwa na hatia kutokana na sababu za ubinafsi mambo ambayo yanatupelekea
kunakosa amani katika familia zetu kwasababu damu za watu zisizokuwa na hatia zinatulilia!
Je, hao wanaofanya vitendo hivyo hawajatokea kwenye wanafamilia zetu au jamii zetu? Mwaka
huu wa imani sisi wanafamilia ya Mungu tunaalikwa kutafari kwa kina wajibu wetu katika
familia na taifa zima la Mungu. Katika kutimiza wajibu wetu kwa Mungu, kwa familia
zetu na kwa taifa zima la Mungu, hatuwezi kufanikiwa vizuri kwa nguvu zetu wenyewe.
Tunahitaji hekima ambayo ni zawadi kutoka kwa Mungu. Tuige mfano mfalme Sulemani aliyepewa
uhuru wa kuchagua zawadi yoyote anayopenda katika maisha naye akachagua hekima ya
kupambanua jema na baya (1 Wafalme 3:9). Katika Kitabu cha (Mithali 9:10) tunaambiwa
kuwa mwanzo wa hekima hiyo ya kweli ni kumcha Mungu. Wapendwa wanafamilia ya Mungu,
huu ni wakati muafaka wa kutafakari tena mahusiano yetu na Mungu, familia zetu na
jamii kwa ujumla, na pale tulipokuwa tumevunja mahusiano hayo kwa namna yoyote tufanye
toba ya kweli na kuanza maisha mapya kusudi tuwe mashahidi wa kweli wa Injili ya Kristu
katika familia zetu na Taifa zima la Mungu. Makala hii imeandaliwa na Padre Titus
Nkane, OSB.