Athari ya baa la njaa ni kubwa zaidi kuliko thata ukosefu wa nguvu mwilini kutokana
na kutopata chakula cha kutosha na chenye madini muhimu ya kuulisha mwili. Athari
hizi hujionesha hasa kwenye sekta za elimu na afya ambapo imebainika kwamba, watoto
wanaokosa chakula na lishe bora hupata shida ya kuelewa vyema masomo shuleni, na hatimaye,
kama watu wazima wanaweza kujikuta wakitupwa pembezoni mwa jamii kwa kutoweza kujimudu
kimaisha kama matokeo ya moja kwa moja ya baa la njaa.
Haya yamejiri
kwenye taarifa ya utafiti wa serikali ya Swaziland iliyowezeshwa na msaada kutoka
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, (WFP).
Utafiti huo
pia unabainisha kwamba, hata uchumi wa Swaziland unaathirika kwa kiasi kikubwa, kwani,
baa la njaa linasababisha upungufu wa Pato Ghafi la Taifa, kwa asilimia 3.1% ambayo
inaweza kulinganishwa na dola za kimarekani milioni 92. Pia kama matokeo ya moja
kwa moja ya ukosefu wa chakula, watoto asilimia 12% wenye umri wa kuwa shuleni hawamalizi
masomo yao, pia asilimia 40% ya wafanyakazi nchini humo wameathiriwa na magonjwa yanayotokana
na ukosefu wa chakula na lishe bora walipokuwa watoto.
Utafiti huo pia umebainisha
kuwa, baa la njaa huwaathiri watoto 46,000 kati ya watoto 156,000 walio chini ya umri
wa miaka 5, au watoto watatu kati ya kila watoto 5 wanaozaliwa. Zaidi ya hayo, ukosefu
wa huduma muhimu unachangia kuongeza kwa athari hizo, kwani asilimia 69% za kesi
za utapiamlo hazipati matibabu.
Kwenye miezi ya hivi karibuni, Swaziland, ambayo
ndiyo nchi ya pekee Barani Afrika iliyo na mfumo wa utawala wa kifalme, imeshuhudia
upinzani kutoka makundi yanayo tetea haki msingi za binadamu na utawala wa kidemokrasia
yanayotaka uhuru wa kujieleza na haki za kibinadamu. Swaziland inasisitiza kufanya
uchaguzi wa wabunge wake kati ya Mwezi Agosti na Septemba, 2013 ijapokuwa upinzani
umetishia kuugomea uchaguzi huo.