Ifuatayo ni hotuba iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, hapo tarehe 31
Julai 2013: wageni waliotembelea Tanzania; Mahakama kuu na changamoto za utekelezaji
wa majukumu yake; ulinzi na usalama; hali ya wakimbizi na wahamiaji nchini Tanzania
na changamoto zilizopo. Rais Kikwete amegusia hali ya uhusiano kati ya Tanzania na
Rwanda ambao kwa sasa unapitia kipindi kigumu. Ninakualika kujitaabisha kusoma ili
ufaidi yale yaliyojiri katika hotuba ya Rais Kikwete, usingoje kuambiwa!
Ndugu
wananchi; Kama ilivyo ada naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa
rehma, kwa kutujalia uzima na kutuwezesha kwa mara nyingine tena kutekeleza utaratibu
wetu huu mzuri tuliojiwekea wa Rais kuzungumza na taifa kila mwisho wa mwezi.
Ndugu
Wananchi; Mwezi Julai, 2013 ulikuwa wa neema kubwa ya wageni kwa nchi yetu wakiwemo
watu na viongozi mashuhuri duniani. Natoa shukrani nyingi kwa Watanzania wenzangu
kwa jinsi tulivyowapokea wageni wetu zaidi ya 1,700. Wamefurahi kuwepo kwao nchini
na wameondoka wakiwa na kumbukumbu nzuri ya nchi yetu. Wageni wetu wamekuwa wa manufaa
makubwa kwa nchi yetu. Wamesaidia kuitangaza Tanzania duniani na kuendeleza fursa
za kukuza utalii, biashara na uwekezaji nchini na kwingineko katika Afrika.
Mkutano
wa Smart Partnership
Ndugu wananchi; Wageni wetu wa kwanza ni wale
waliokuja kuhudhuria Mkutano wa Global 2013 Smart Partnership Dialogue uliofanyika
Dar es Salaam tarehe 28 Juni hadi 1 Julai, 2013. Mkutano huo ulihudhuriwa na
watu zaidi ya 800 kutoka mabara yote duniani wakiwemo Watanzania. Miongoni mwa waliohudhuria
ni pamoja na wakuu wa nchi na Serikali, viongozi wastaafu, wanadiplomasia, wawakilishi
wa mashirika na taasisi za kimataifa, makampuni ya ndani na nje, wafanyabiashara,
wasomi, asasi za kijamii na watu wa makundi mbalimbali katika jamii. Makampuni yetu
21 nayo yaliungana na makampuni mengine 28 kutoka nje ya nchi kushiriki kwenye maonesho
ya matumizi ya sayansi na teknolojia yaliyofanyika sambamba na mkutano huo.
Ndugu
Wananchi; Agenda kuu ya majadiliano ya mwaka huu ilikuwa ni “Matumizi ya teknolojia
kama nyenzo ya kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi Barani Afrika (Leveraging Technology
for Africa’s Social-Economic Transformation: The Smart Partnership Way). Tuliichagua
mada hii kwa kuwa ni ukweli ulio wazi kuwa matumizi ya sayansi na teknolojia ndiyo
chachu kubwa iliyoleta mageuzi na maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi. Ndiyo
siri ya mafanikio katika nchi zilizoendelea na zinazopiga kasi kubwa ya maendeleo
duniani.
Bahati mbaya sana kumekuwa na maendeleo na matumizi madogo ya sayansi
na teknolojia katika Afrika. Ndiyo maana nchi za Afrika ziko nyuma kimaendeleo ukilinganisha
na zile zilizoendelea. Katika mkutano huo umuhimu wa kuendeleza na kuongeza matumizi
ya sayansi na teknolojia kwa ajili ya maendeleo Barani Afrika ulitambuliwa na kusisitizwa.
Mkutano
ulihimiza na kusisitiza kuwa sera, mikakati na mipango ya maendeleo ya nchi za Afrika
zitoe kipaumbele kwa kuendeleza matumizi ya sayansi na teknolojia. Nchi zetu zimehimizwa
kuwekeza katika elimu ya sayansi na teknolojia pamoja na kujenga uwezo wetu wa ndani
wa uvumbuzi, ubunifu, umiliki na uendelezaji wa sayansi na teknolojia. Aidha, imesisitizwa
kwa nchi zetu ziongeze kasi ya kutumia sayansi na teknolojia katika shughuli mbalimbali
za kiuchumi na kijamii ili kuongeza ufanisi na kasi ya maendeleo.
Ndugu Wananchi; Jambo
la kutia faraja kwetu nchini ni kwamba mambo yote hayo tunayafanya. Tunachotakiwa
sasa ni kufanya vizuri zaidi na kuongeza uwekezaji na kasi ya kuendeleza matumizi
ya sayansi na teknolojia katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Tutaendelea kuboresha sera, kuboresha mazingira ya uwekezaji na kwa ajili ya maendeleo
ya sayansi na teknolojia nchini.
Ziara ya Rais wa Marekani Nchini Tanzania
Ndugu
wananchi; Mgeni wetu wa pili alikuwa Rais wa Marekani, Mheshimiwa Barack Obama,
aliyefanya ziara nchini kwetu kati ya tarehe 1 - 2 Julai, 2013. Lengo la ziara yake
ilikuwa kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya Marekani na Tanzania. Kama
mjuavyo, nchi zetu mbili zina uhusiano wa kibalozi tangu Uhuru wa Tanganyika mwaka
1961 na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar mwaka 1964.
Uhusiano wetu umepita katika
vipindi mbalimbali na kwamba hivi sasa umekuwa mzuri zaidi kuliko wakati mwingine
wowote katika historia ya nchi zetu mbili. Kumekuwepo na ongezeko kubwa la misaada
ya maendeleo kutoka Marekani na uwekezaji wa vitega uchumi na biashara navyo vinakua.
Pia ziara za kiserikali za viongozi wa nchi zetu kutembeleana zimeongezeka. Kama mtakavyokumbuka,
mwaka 2008 aliyekuwa Rais wa Marekani Mheshimiwa George W. Bush alifanya ziara ya
siku nne nchini. Pia Mawaziri mbalimbali wa Serikali ya Marekani wametembelea Tanzania
akiwemo Mheshimiwa Hilary Clinton akiwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani aliyekuja
mwaka 2011.
Ndugu Wananchi; Nchi ya Marekani imekuwa mshirika wetu
muhimu wa maendeleo katika nyanja mbalimbali. Kwa upande wa afya kwa mfano, tunapata
msaada mkubwa katika mapambano dhidi ya malaria na UKIMWI. Katika maendeleo ya elimu,
nako wanatusaidia katika mafunzo ya wataalamu mbalimbali pamoja na upatikanaji wa
vitabu vya sayansi na hisabati kwa ajili ya shule za sekondari. Kupitia Mfuko wa
Changamoto za Milenia, Marekani inatusaidia katika kuimarisha miundomuinu ya barabara,
umeme na maji.
Ujenzi wa barabara za Tanga – Horohoro, Namtumbo – Songea
– Mbinga; Tunduma – Sumbawanga na baadhi ya barabara za Pemba, ujenzi wa njia ya pili
ya kupeleka umeme Unguja kutoka Dar es Salaam, ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mafia
na usambazaji wa umeme katika Mikoa 10 ya Tanzania bara ni miongoni mwa matunda ya
msaada wa Mfuko huo. Pamoja na hayo, ipo miradi ya kuongeza maji katika jiji la Dar
es Salaam na Manispaa ya Morogoro ambayo inaendelea kutekelezwa.
Ndugu Wananchi; Wakati
wa ziara yake, Rais Obama alielezea na kusisitiza dhamira yake na ya Serikali yake
ya kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi zetu. Alielezea
kuridhika na hatua tuliyofikia ya kukuza demokrasia nchini, utawala bora na kuwekeza
katika maendeleo ya watu wetu. Aliahidi kuendelea kuunga mkono juhudi zetu. Katika
hili ameahidi kuongeza misaada ya maendeleo na kiufundi katika sekta za afya, elimu,
kilimo, barabara, nishati na maendeleo ya vijana.
Pia, alithibitisha kwamba
nchi yetu itaendelea kunufaika na ufadhili wa Awamu ya Pili ya Mfuko wa Changamoto
za Millenia. Katika awamu hii, maeneo yatakayopewa kipaumbele hapa kwetu ni umeme
na barabara za vijijini. Mazungumzo ya miradi itakayotekelezwa katika awamu hiyo
yanaendelea vizuri.
Power Africa
Ndugu Wananchi; Rais
Obama alitumia fursa ya ziara yake nchini kuzindua mpango wa Serikali yake wa kusaidia
maendeleo ya sekta ya umeme katika Bara la Afrika. Mpango huu unaoitwa “Power Africa
Initiative” umetengewa kiasi cha dola za Marekani bilioni 7 na Serikali ya Marekani
na makampuni binafsi ya nchi hiyo yameahidi kuwekeza dola bilioni 9 katika mpango
huo. Kwa kuanzia, nchi sita za Afrika (Ethiopia, Ghana, Nigeria, Tanzania, Liberia
na Kenya) ikiwemo Tanzania zitahusishwa.
Bila ya shaka Mpango huo ukikamilika
utasaidia sana kuimarisha upatikanaji wa umeme barani Afrika ambayo ni nyenzo muhimu
katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Ni ukweli ulio wazi kuwa ukosefu
wa umeme wa kutosha na wa uhakika ni sababu kubwa inayokwamisha maendeleo ya haraka
katika nchi za Afrika. Hivyo basi, msaada huu ni muhimu sana kwetu. Kwa ajili hiyo
nimeagiza Wizara ya Nishati na Madini iandae mkakati madhubuti wa namna Tanzania itakavyoshiriki
na kufaidika na mpango huo. Nataka mpango huo utakapoanza kutekelezwa utukute sisi
tupo tayari kutumia fursa zake.
Vile vile, ndugu wananchi, katika ziara hiyo
Rais Obama alielezea nia ya Serikali yake kutaka kuwepo mpango wa kukuza ushirikiano
wa biashara na uwekezaji baina ya nchi yake na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Nimeelekeza Wizara husika yaani Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara
ya Viwanda, Biashara na Masoko nao watengeneze mkakati utakaoonesha jinsi tulivyojipanga
kufaidika na mpango huo. Lazima tujiandae vyema na mapema tunufaike saiwa na mpango
huo.
Ziara ya Rais Mstaafu wa Marekani Nchini
Ndugu Wananchi; Sambamba
na ziara ya Rais Obama, nchi yetu ilipata bahati ya kutembelewa tena na Rais Mstaafu
wa Marekani, Mheshimiwa George W. Bush na mkewe Laura Bush, tarehe 1 hadi 3 Julai,
2013. Kwa udhamini wa asasi ya George W. Bush Foundation waliandaa Mkutano wa Wake
wa Marais wa Afrika uliofanyika hapa Dar es Salaam, tarehe 2 na 3 Julai, 2013. Mama
Michelle Obama naye alishiriki mkutano huo uliozungumzia kuimarisha maendeleo na afya
ya wanawake Barani Afrika.
Katika mkutano huo, pia, Mheshimiwa George W. Bush
alizindua mpango wa kuimarisha mapambano dhidi ya kansa ya shingo ya kizazi na matiti
barani Afrika. Kufuatia Mpango huo, Serikali ya Marekani imetoa dola milioni 3 na
mashine 16 za Cryo Therapy zinazotumia baridi kali kuua chembechembe za kansa. Msaada
huo ni muhimu hasa ukizingatia kuwa kila mwaka hapa nchini zaidi ya Watanzania 21,000
wanapata maradhi ya kansa. Kati ya hao asilimia 29.4 ni wanawake wanaopata magonjwa
ya kansa ya shingo ya uzazi na asilimia 6.2 wanapata kansa ya matiti. Naamini Mpango
huu utatusaidia sana katika kuimarisha mapambano dhidi ya maradhi haya yanayowasumbua
na kuua kina mama wengi nchini. Nimeitaka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuweka
utaratibu mzuri ili msaada huo utumike ipasavyo na kuwanufaisha walengwa.
Ziara
ya Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza Nchini
Ndugu Wananchi; Tarehe
23 mwezi Julai, 2013 pia tulitembelewa na Waziri Mkuu Mstaafu wa Uingereza, Mheshimiwa
Tony Blair. Katika mazungumzo yetu Mheshimiwa Blair aliahidi kuisaidia nchi yetu
kupitia taasisi yake ya Africa Governance Initiative kusaidia kusambaza umeme wa jua
katika shule zetu za sekondari vijijini, maboresho ya shirika letu la umeme (TANESCO)
na kusaidia uanzishaji na uimarishaji wa Kitengo cha Rais cha Ufuatiliaji Utekelezaji
wa Programu za Maendeleo (Presidential Delivery Bureau - PDB). Tunamshukuru kwa
ahadi yake hiyo itakayochangia katika jitihada za kujiletea maendeleo.
Ziara
ya Waziri Mkuu wa Thailand Nchini
Ndugu Wananchi; Tarehe 30 Julai,
2013 tulimpokea Mheshimiwa Yingluck Shinawatra, Waziri Mkuu wa Thailand aliyefanya
ziara ya siku tatu nchini. Lengo la ziara yake ni kuimarisha uhusiano mzuri uliopo
kati ya Thailand na Tanzania. Katika ziara hiyo, tumezindua Jukwaa la Wafanyabiashara
wa Thailand na Tanzania (Thai-Tanzania Business Forum) ili kukuza biashara na uwekezaji
baina ya nchi zetu. Waziri Mkuu Yingluck Shinawatra alitumia fursa hiyo kufafanua
sera ya Thailand kwa Afrika inayosisitiza kukuza ushirikiano wa karibu wa kiuchumi
na kibiashara. Pia amepata nafasi ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kujionea
mwenyewe jinsi nchi yetu ilivyobarikiwa kwa kuwa na kivutio hicho cha aina yake.
Alipokuwa kule nchi zetu zilitiliana saini maelewano ya ushirikiano katika kulinda
na kuhifadhi wanyama pori.
Katika mazungumzo yangu na yeye, tumekubaliana kuchukua
hatua thabiti kukuza ushirikiano katika nyanja mbalimbali. Tumetiliana saini mikataba
mitano ya ushirikiano kwa mambo yafuatayo: Kukuza na kulinda vitega uchumi; kubadilishana
wafungwa; ushirikiano wa kiufundi; na ushirikiano kwa masuala ya madini. Aidha, Waziri
Mkuu huyo ameahidi kuwahimiza wawekezaji wa nchini mwake kuja Tanzania kuwekeza katika
sekta mbalimbali za uchumi ikiwemo kilimo, utalii, viwanda nakadhalika.
Pia,
Waziri Mkuu wa Thailand ameahidi kuwa Serikali yake itatoa ufadhili kwa vijana 10
kusoma Shahada ya Uzamili nchini humo. Vile vile, nchi hiyo itaanza kuleta wataalamu
wa afya wa kujitolea kuja kushirikiana na wataalam wetu kuimarisha huduma ya afya
nchini. Ziara hizi zinaonesha utayari wa dunia kuunga mkono jitihada zetu za
kujiletea maendeleo. Naomba Watanzania wenzangu tutumie vizuri utayari huo wa dunia
kuongeza kasi ya maendeleo yetu. Tusijikwaze wenyewe.
Ziara ya Kagera
Ndugu
wananchi; Kuanzia tarehe 24 hadi 29 Julai, 2013, nilifanya ziara Mkoani Kagera.
Nilishiriki kwenye Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa na kuzindua jengo jipya la Mahakama
Kuu. Pia niliweka jiwe la msingi la upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Bukoba na kuweka
mawe ya msingi ya ujenzi wa kiwango cha lami kwa barabara za Kigoma – Lusahunga na
Kyaka – Kayanga – Bugene. Vile vile nilizindua Wilaya mpya ya Kyerwa na kukagua shughuli
za maendeleo pamoja na kuona na kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi
ili kuzitafutia majawabu.
Sherehe za Kumbukumbu ya Mashujaa zilifana sana.
Niliwapongeza viongozi wa Jeshi na wa Mkoa kwa maandalizi mazuri ya sherehe hizo.
Pia nilirudia kumpongeza Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange, kwa uamuzi wake
wa busara wa kufanya sherehe za kumbukumbu za mashujaa wetu pale Kaboya badala ya
kufanyikia Dar es Salaam tu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Ni uamuzi muafaka
na wa busara kwani pale Kaboya ndipo walipolala mashujaa wetu waliopoteza maisha
yao kutetea mipaka na uhuru wa nchi yetu dhidi ya Nduli Iddi Amin. Hali kadhalika,
kule Naliendele, Mtwara ambapo sherehe za mashujaa zilifanyika mwaka wa juzi, ndipo
walipozikwa mashujaa wetu waliopoteza maisha kuisaidia nchi jirani na rafiki ya Msumbuji
kutetea Uhuru wake dhidi ya wakoloni, makaburu na vibaraka wao wa ndani ya Msumbiji.
Ndugu
Wananchi; Katika hotuba yangu pale Kaboya niliwakumbusha Watanzania wenzangu kwamba
katika kuwakumbuka mashujaa wetu wale na sisi tulio hai, hatuna budi kutambua wajibu
wetu wa kuwa tayari kujitolea muhanga kwa ajili ya kulinda uhuru wa mipaka ya nchi
yetu. Nilisisitiza utayari wa nchi yetu kulinda mipaka yake na kwamba mfano wa mashujaa
waliolala pale ni fundisho kwa mtu ye yote anayetamani kumega kipande cho chote cha
ardhi ya nchi yetu. Atakiona cha mtema kuni kilichomkuta Nduli Iddi Amini au hata
zaidi.
Nimesikia kuwa kauli yangu ile imetafsiriwa visivyo na kupotoshwa na
baadhi vyombo vya habari na hata majirani zetu. Tafsiri hizo ni potofu. Sikumtaja
mtu ye yote au nchi yo yote. Nilikuwa nazungumzia wajibu wa majeshi yetu na raia
wa nchi yetu wa kulinda uhuru na mipaka yetu na kwamba hatutamruhusu mtu au nchi yo
yote kutupokonya wala kuichezea haki yetu hiyo ya msingi. Tuko tayari kuitetea hata
kama gharama yake ni maisha yetu kama walivyofanya mashujaa waliolala Kaboya.
Mahakama
Kuu
Ndugu Wananchi; Katika ufunguzi wa Mahakama Kuu ya Bukoba nilisisitiza
dhamira na utayari wa Serikali yetu kuiwezesha Mahakama ya Tanzania kuwa na Mahakama
Kuu katika kila Mkoa. Baada ya kukamilika kwa Mahakama Kuu ya Bukoba bado kuna Mikoa
14 hainazo. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2013/14 tumetenga fedha za kujenga Mahakama
Kuu katika Mikoa 7 na nilirudia ahadi yangu kuwa katika mwaka ujao wa fedha tutatoa
fedha za kumalizia Mikoa 7 iliyosalia. Niliamua tuongeze kasi ya kujenga Mahakama
Kuu hizo ili kuiwezesha Mahakama ya Tanzania kutimiza ipasavyo wajibu wake wa kutoa
haki nchini.
Maendeleo ya Mkoa wa Kagera
Ndugu Wananchi; Nilipokuwa
Kagera nilifurahishwa na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi
na kijamii. Taarifa za Mkoa na Wilaya zimefafanua kwa kina mambo mazuri yaliyofanyika
na yanayoendelea kufanyika Mkoani. Wameelezea furaha yao kwa mafanikio yaliyopatikana
ambayo baadhi nimeyashuhudia au hata kushiriki kuyazindua na kuweka mawe ya msingi.
Taarifa hizo pia zimelezea mambo mengi zaidi wanayotaka yafanyike na matatizo mapya
na hata ya zamani ambayo wanataka yapatiwe ufumbuzi. Katika mazungumzo yangu na
viongozi na wananchi, yapo mambo ambayo yako kwenye uwezo wao kijijini, Wilayani na
Mkoani kuyapatia ufumbuzi. Tulikubaliana na kuelekezana nini kifanyike. Yapo mengine
mengine ambayo yanahitaji nguvu ya taifa tumeyachukua kuja kuyafanyia kazi. Kuna
baadhi yaliwahusu Mawaziri ambao nilikuwa nao ziarani waliyasemea na kuyafanyia kazi
palepale yalipojitokeza.
Ulinzi na Usalama
Ndugu Wananchi; Kuna
mambo matatu yahusuyo usalama ambayo yalizungumzwa na wananchi kwa uchungu mkubwa
ambayo niliamua tuyashughulikie kitaifa. Mambo hayo ni ujambazi wa kutumia silaha
kuteka magari, kupora mali na watu kuuawa. Jambo la pili ni wahamiaji kutoka nchi
jirani wanaoingia, kuishi na kufanya shughuli nchini kinyume cha sheria. Na tatu,
mifugo kuingizwa kwa wingi nchini bila kufuata taratibu husika na mingine kuingizwa
katika hifadhi za wanyama.
Ndugu wananchi; Nilitoa maagizo kwa wakuu wa
vyombo vya ulinzi na usalama yaani JWTZ, Polisi, Usalama wa Taifa na Uhamiaji watengeneze
mpango kabambe wa kuyashughulikia matatizo hayo. Watayarishe na kutekeleza operesheni
maalum itakayo au zitakazokomesha ujambazi, kuondoa wahamiaji wasiokuwa halali na
kuondoa mifugo iliyoingizwa nchini kinyume na utaratibu na ile iliyoko kwenye maeneo
yasiyo stahili.
Aidha, niliwataka majambazi wajisalimishe na wasalimishe silaha
zao ndani ya wiki mbili na siku hizo zinaanzia tarehe 29 Julai, 2013 nilipomaliza
ziara yangu Mkoani humo. Kwa wahamiaji wanaoishi nchini kinyume cha sheria nimewataka
watumie muda huo kuondoka nchini au kuhalalisha ukaazi wao. Hivyo hivyo kwa mifugo
iliyoingizwa nchini kinyume na sheria au ile iliyoko kwenye maeneo yasiyostahili.
Ndani ya muda huo watu wote waondoe mifugo yao au wajitokeze kufuata taratibu zilizopo.
Ndugu
Wananchi; Nilisema nilipokuwa Mkoani Kagera na narudia tena leo kuwa baada ya siku
14 kupita, vyombo vya ulinzi na usalama vitaendesha operesheni maalum ya kushughulikia
matatizo hayo. Nilisema kuwa operesheni hiyo itafanyika katika Mikoa ya Kigoma, Kagera
na Geita kwa wakati mmoja. Napenda kuwahakikishia kuwa hapatakuwa na mahali pa kukimbilia
wala kujificha. Nawashauri wale wote wanaohusika na ujambazi, uhamiaji haramu na
uingizaji haramu wa mifugo waamue kuchukua hatua muafaka sasa. Wasisubiri operesheni
iwakute, wala wasifikirie kuwa hili ni jambo la kupita. Safari hii itakuwa endelevu.
Ndugu
Zangu; Hatuwezi kukubali hali hii niliyoikuta Mkoani Kagera ikaachwa kuendelea.
Italeta madhara makubwa zaidi siku za usoni. Haiwezekani raia katika nchi yake, akose
uhuru na usalama wa kutembea peke yake mpaka asindikizwe na Polisi. Na, baya zaidi
hata Polisi nao wanashambuliwa na kuuawa watakavyo majambazi. Uhalifu huu lazima
ukomeshwe, uishe na usijirudie tena.
Pia, haiwezekani hali ya watu kutoka nchi
jirani kuingia nchini, kuishi na kufanya shughuli na kutoka watakavyo. Hatuzuii watu
kuingia na kuishi Tanzania lakini wafuate sheria na taratibu za kuhamia na kuishi
katika nchi yetu. Nchi yetu ina sifa na ukarimu huo. Hakuna uthibitisho mkubwa zaidi
ya ule wa mwaka 1982, Rais Julius Nyerere wakati ule alipowaruhusu wakimbizi wanaopenda
kuwa raia wa Tanzania wafanye hivyo. Wakimbizi 30,000 tu waliitumia fursa hiyo.
Mwaka 2010 tuliwapa uraia wakimbizi 160,000 wa kutoka Burundi. Kwa sababu hiyo hatuoni
sababu ya watu kufanya wanayoyafanya sasa kule Mkoani Kagera. Hatuwezi kuacha hali
hiyo iendelee ilivyo.
Ndugu Wananchi; Nilipokuwa Mkoani Kagera nilielezea
kusikitishwa kwangu na vitendo vya baadhi ya watendaji na viongozi wa vijiji na wananchi
kuwaruhusu watu kuingia na kuishi nchini kinyume cha sheria. Nimewataka waache mtindo
huo. Nimeagiza na wao wajumuishwe katika operesheni ijayo. Watakaobainika kujihusisha
na vitendo hivyo haramu wachukuliwe hatua zipasazo kisheria. Aidha, niliwataka Maafisa
wa Uhamiaji watimize ipasavyo wajibu wao. Ukweli ni kwamba, mambo haya kuendelea
kwa muda mrefu kiasi hiki ni kwa sababu ya udhaifu wa mamlaka husika. Vile vile,
nimewataka TAKUKURU nao watimize wajibu wao. Hapa kuna uthibitisho tosha wa kuwepo
kwa vitendo vya rushwa vinavyohusisha wahamiaji hao na maofisa wa vijiji na idara
husika za Serikali. Mimi naamini kama TAKUKURU ikiwabana na Uhamiaji wakichemka vya
kutosha tatizo hili lingepungua sana au hata kutokuwepo kabisa.
Uhusiano
na Nchi ya Rwanda
Ndugu wananchi; Katika kipindi cha miezi miwili
sasa hususan tangu mwishoni mwa mwezi Mei, 2013, uhusiano baina ya nchi yetu na Rwanda
unapitia katika wakati mgumu. Kauli za viongozi wa Rwanda dhidi yangu na nchi yetu
ni ushahidi wa kuwepo hali hiyo. Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu na ndugu
zetu wa Rwanda kuwa mimi, Serikali ninayoiongoza na wananchi wa Tanzania tunapenda
kuwa na uhusiano mzuri na ushirikiano wa karibu na Rwanda kama ilivyo kwa nchi zote
jirani. Kama majirani kila mmoja anamuhitaji mwenzake, hivyo lazima tuwe na uhusiano
mwema na ushirikiano mzuri.
Napenda kusisitiza kuwa mimi na Serikali ninayoiongoza
tutakuwa wa mwisho kufanya kitendo au vitendo vibaya dhidi ya Rwanda au nchi yo yote
jirani au yo yote duniani. Hatuna sababu ya kufanya hivyo kwani ni mambo ambayo hayana
tija wala maslahi kwetu.
Ndugu Wananchi; Ukweli ni kwamba wakati wote tumekuwa
tunajihusisha na mambo ya kukuza na kujenga ujirani mwema na kufanya mambo ambayo
yatasaidia kuimarisha uhusiano wetu kwa maslahi ya nchi zetu. Hiyo ni moja ya nguzo
kuu ya Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania. Huo ndiyo ukweli kuhusu uhusiano wetu na
nchi ya Rwanda kabla na hata baada ya sintofahamu iliyojitokeza sasa.
Napenda
kuwahakikishia ndugu zetu wa Rwanda kuwa kwa upande wetu hakuna kilichobadilika wala
kupungua katika uhusiano na ushirikiano wetu. Mambo yapo vile vile. Kwa upande wangu,
binafsi, sijasema lo lote kuhusu Rwanda pamoja na maneno mengi ya matusi na kejeli
yanayotoka kwenye vinywa vya viongozi wa Rwanda dhidi yangu. Siyo kwamba siambiwi
yanayosemwa au sijui kusema au sina la kusema, la hasha. Sijafanya hivyo kwa sababu
sioni faida yake. Kwangu mimi sioni kama kuna mgogoro wa aina yo yote. Busara inatuelekeza
kuwa tusikuze mgogoro usiokuwepo. Waingereza wanasema “two wrongs do not make a right”.
Ndugu
Wananchi; Kama mjuavyo uhusiano wetu na Rwanda umekuwa mzuri kwa miaka mingi.
Tunashirikiana na kusaidiana kwa mambo mengi baina ya nchi zetu kitaifa na katika
kanda yetu ya Afrika Mashariki na Nchi za Maziwa Makuu, katika Umoja wa Afrika na
hata kimataifa. Uhusiano unaelekea kupata mtikisiko baada ya mimi kutoa ushauri kwa
Serikali ya Rwanda kuzungumza na mahasimu wao. Ushauri ule niliutoa kwa nia njema
kabisa kwani bado naamini kuwa kama jambo linaweza kumalizwa kwa njia ya mazungumzo
njia hiyo ni vyema itumike. Isitoshe, ushauri ule niliutoa pia kwa Serikali ya Kongo
na kwa Serikali ya Uganda. Katika mkutano ule Rais Yoweri Museveni wa Uganda aliunga
mkono kauli yangu. Rais wa Rwanda hakusema cho chote pale mkutanoni. Baada ya kurudi
nyumbani ndipo tukaanza kuyasikia maneno tuliyoyasikia na tunayoendelea kuyasikia.
Kwa
kweli nimestaajabu sana na jinsi walivyouchukulia ushauri wangu na wanayoyafanya.
Havifanani kabisa, completely out of proportion and out of context. Mimi nilifanya
vile kwa kuzingatia mila na desturi zetu za miaka mingi katika ukanda wetu. Tumekuwa
tunakutana katika mikutano na vikao mbalimbali tunazungumza na kushauriana kwa uwazi
juu ya njia za kushughulikia matatizo na masuala mbalimbali kila yanapotokea. Wakati
wote tumeyachukulia kuwa ni mambo yanayotuhusu sote hivyo kupeana ushauri ni wajibu
wetu wote.
Na mara nyingi ushauri kwa wanaogombana kuzungumza tunautumia
sana. Iweje leo mtu kutoa ushauri ule lionekane jambo baya na la ajabu. Jambo la
kushutumiwa na kutukanwa! Siyo sawa hata kidogo!! Ushauri si shuruti, ushauri si
amri. Una hiyari ya kuukubali au kuukataa. Muungwana hujibu: “Siuafiki ushauri
wako”. Hakuna haja ya kutukana wala kusema maneno yasiyostahili wala kusema yasiyokuwepo
na ya uongo.
Ndugu Wananchi; Napenda kurudia kusema kuwa mimi binafsi na
Serikali yetu ya Tanzania hatuna ugomvi wala nia yo yote mbaya na Rwanda. Tunapenda
tuendelee kuwa na uhusiano mzuri na Rwanda. Labda wenzetu wanalo lao jambo dhidi
yetu ambalo sisi hatulijui. Maana na sisi tunasikia mengi yanayozungumzwa na kudaiwa
kupangwa kufanywa na Rwanda dhidi yangu na nchi yetu. Hatupendi kuyaamini moja kwa
moja tunayoyasikia lakini hatuyapuuzi.
Ndugu Wananchi; Kabla ya kumaliza,
naomba kutumia nafasi hii pia kuwatakia Waislamu wote nchini heri na baraka tele katika
kukamilisha ibada muhimu ya kufunga mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Naomba tuendelee kuwatakia
heri ili wamalize salama na tuweze kusherehekea kwa furaha na bashasha tele siku kuu
ya Idd el Fitr pindi itakapowadia.
Mwisho kabisa, nawaomba Watanzania wenzangu
wote tuendelee kushirikiana na kuishi kwa upendo, umoja na mshikamano kama ilivyo
kawaida yetu.
Mungu Ibariki Tanzania! Mungu Ibariki Afrika! Asanteni
Sana Kwa Kunisikiliza.