2013-08-03 14:46:27

Wahudumieni wananchi wa Kenya kwa ari na moyo mkuu bila ubaguzi!


Askofu Mkuu Zacchaeus Okoth wa Jimbo kuu la Kisumu nchini Kenya ameiomba Serikali ya Kenya kuonesha ukakamavu wake katika kuwahudumia wananchi wote kwa usawa pasipo ubaguzi wa aina yoyote ile.

Askofu Mkuu Okoth, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Nchini Kenya, amesema ni muhimu kwa wabunge na wawakilishi wa wilaya, viongozi waliochaguliwa kwa kupigiwa kura na wananchi, kuhakikisha wanayajali maslahi ya Wakenya wote kwa ujumla, na kutoa huduma bora ambazo zitachangia katika uboreshaji wa maisha ya wananchi wote.

Amesikitika kuona kwamba wabunge walionesha tamaa isiyo na kifani, walipoamua kujiongezea mishahara yao kinyume na mapendekezo ya Serikali na yale ya kamati ya kurekebisha mishahara na malipo kwa wafanyakazi wa umma.

Askofu mkuu Okoth alikuwa akiongea na waandishi wa habari baada ya kukamilisha mkutano wa Tume ya haki na amani kwenye Kituo cha Kolping, kilichoko mjini mjini Thika. Mkutano huo ulihudhuriwa na wawakilisha kutoka majimbo 23 kati ya majimbo 26 yanayounda Kanisa Katoliki nchini Kenya.

Askofu Okoth alionyesha masikitiko yake kutokana na kile alichokiita vitendo vya maafisa wa usalama kuwashika na kuwahoji, kuwadhalilisha na hata kuwatesa watu wanaoaminika kuwa na maoni tofauti ya kisiasa. Anasema kwamba, nchi hiyo bado ina kumbukumbu ya yale yaliyojiri siku za nyuma ambapo watu wengi waliteswa kwa kuonesha misimamo iliyoonekana kupingana na ile ya serikali, kitu ambacho ni kinyume na roho ya Katiba inayompa kila mtu uhuru wa kuwa na maoni na misimamo yake kisiasa.

Askofu mkuu Zacchaeus Okoth anasema ni sharti Katiba na sheria zizingatiwe vilivyo ili haki na amani vidumu katika utekelezaji wote wa shughuli za kiserikali.








All the contents on this site are copyrighted ©.