Kardinali Stanislaw Dziwisz, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cracovia, mwenyeji wa Maadhimisho
ya Siku ya 29 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 amezindua mtandao kwa ajili ya Maadhimisho
ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 kwa lugha ya Kiingereza. Unaweza kuperuzi
kwenye mtandao huo kwa anuani ifuatayo: www.krakow2016.com.
Maadhimisho haya
yatakuwa ni nafasi ya pekee kwa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwa ajili
ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa matendo makuu aliyolikirimia
Kanisa lake kwa njia ya maisha na utume wa Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, aliyewapenda
vijana upeo na wakamwonesha kwamba, kwa hakika walikuwa wamemkubali, kiasi hata cha
kupiga ukelele atangazwe kuwa mtakatifu mara moja!
Mwenyeheri Yohane Paulo
wa Pili ni urithi mkubwa katika maisha na utume Kanisa. Ni kiongozi aliyeonesha utakatifu
wa maisha na akawa ni mfano wa kuigwa miongoni mwa vijana kiasi cha kujitosa bila
ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani, huku wakiendeleza na kudumisha Ibada kwa
Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.
Kardinali Stanislaw anasema, Jimbo la
Cracovia, kumekucha! Tayari waamini na wananchi wenye mapenzi mema, wameanza kujiandaa
kwa ajili ya kuwapokea, kuwakaribisha na kuwakirimia vijana kutoka sehemu mbali mbali
za dunia. Anasema, wanajiandaa kujitosa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya vijana
duniani, katika hali ya upendo, ukarimu, udugu na mshikamano wa upendo, ili kuwajengea
vijana matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.