2013-08-03 08:22:26

Kanisa Katoliki Japan linawakumbuka wahanga wa Vita kuu ya Pili ya Dunia


Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani, kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 9 Agosti 2013 atakuwa na ziara ya kichungaji nchini Japan, ili kusali na kutafakari pamoja na Kanisa Katoliki nchini Japan wanapowakumbuka wahanga wa mashambulizi ya kinyuklia yalitokea Hiroshima na Nagasaki, wakati wa vita kuu ya pili ya dunia kunako mwaka 1945.

Hija hii ya kichungaji inakwenda sanjari na Maadhimisho ya Siku Kumi za Amani zilizotangazwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Japan, kuanzia tarehe 6 hadi tarehe 15 Agosti 2013 kama njia ya kuwakumbuka waliopoteza maisha na kuathirika katika mashambulizi ya mabomu ya Atomiki nchini Japan, ambako hata leo hii, madhara yake bado yanaonekana.

Akiwa nchini Japan, Kardinali Turkson atashiriki katika Ibada ya Misa takatifu; Majadiliano ya kidini na waamini wa dini kuu nchini Japan kwa kuonesha umuhimu wa kushirikiana kama njia ya kusimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani duniani.

Kardinali Turkson anatarajiwa kushiriki katika majadiliano ya amani yaliyoandaliwa na Kituo cha Majadiliano ya Kidini mjini Nagasaki na baadaye atashiriki pia katika Maadhimisho ya Mji wa Nagasaki kwa ajili ya kuwakumbuka waathirika wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia nchini Japan, tukio linalotarajiwa kuwashirikisha waamini kutoka katika dini mbali mbali nchini Japan.

Kardinali Turkson, akiwa mjini Nagasaki, tarehe 9 Agosti 2013, atashiriki katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea amani duniani. Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 1981, Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili alipotembelea Hiroshima, alikemea vita na kutaka amani iweze kutawala katika maisha na mioyo ya watu duniani.

Papa Yohane Paulo wa Pili, wakati huo, aliwataka viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kupinga vita kwani vita haijawahi kutatua matatizo na changamoto zinazowakabili watu wa mataifa na badala yake, imekuwa ni chanzo cha taabu na mahangaiko ya watu wengi wasiokuwa na hatia. Vijana wanachangamotishwa kwa namna ya pekee, kuhakikisha kwamba, wanakataa na kupinga matumizi ya vita, kwani mara nyingi wao ndio wanaokuwa wa kwanza kupelekwa mstari wa mbele.

Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili anawaalika vijana kujenga na kuimarisha mshikamano wa upendo na udugu, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu wote. Tangu wakati huo, Baraza la Maaskofu Katoliki Japan, limeendelea kuhamasisha Jamii kujikita katika misingi ya haki na amani, daima wakitambua kwamba, amani na utulivu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayowashirikisha binadamu, lakini kwa namna ya pekee viongozi wa nchi kwani wao wanachukua dhamana na maamuzi makubwa kwa ajili ya wananchi wao.

Jamii ya Kimataifa inahamasishwa kuwa ni wajenzi na vyombo vya amani kwa kuachana na dhana ya vita ambayo kimsingi inaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu wasiokuwa na hatia. Baraza la Maaskofu Katoliki Japan linaendelea kuadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu Mwenyeheri Yohane wa XXIII alipochapisha Waraka wa kichungaji, Pacem in Terris, Amani Duniani. Ni Waraka unaofafanua dhamana na haki ya kila mtu; jukumu la Serikali katika kutafuta na kuendeleza mafao ya wengi.

Ni Waraka unaopembua kwa kina na mapana kuhusu: ukweli, haki, mshikamano, tatizo la wakimbizi, mchakato wa kudhibiti biashara ya silaha duniani; uchumi na maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji msingi ya binadamu kiroho na kimwili. Amani ni fadhila kwa ajili ya binadamu wote inayopaswa kujikita katika ukweli, upendo na uhuru. Ili kudumisha amani, kuna haja ya kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu na kwamba, amani ni kikolezo kikubwa cha maendeleo endelevu kinachopania kujenga na kuimarisha Jamii inayojipambanua katika misingi ya kiutu!All the contents on this site are copyrighted ©.