2013-08-03 11:56:10

Dumisheni amani na utulivu wakati mkisubiri matokeo rasmi ya uchaguzi mkuu


Tume ya haki na amani ya Shikirisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika, IMBISA, inawataka waamini na wananchi wa Zimbabwe katika ujumla wao kuhakikisha kwamba, wanaendeleza amani na utulivu, wakati huu wanaposubiri Tume ya Uchaguzi Zimbabwe kutangaza matokeo rasmi ya uchaguzi mkuu uliofanyika hivi karibuni.

IMBISA inaishauri Tume ya Uchaguzi Zimbabwe kujitahidi kutangaza matokeo ya uchaguzi mkuu, kadiri ya taratibu na sheria za nchi. Hadi sasa IMBISA imeridhika na mchakato mzima wa uchaguzi mkuu nchini Zimbabwe kwa Mwaka 2013. Amani na utulivu vimetawala maeneo mengi, ikilinganishwa na chaguzi zilizopita. Wananchi waliendelea kuonesha utulivu hata pale vituo vya kupigia kura vilipochelewa kufunguliwa kadiri ya ratiba.

Katika uchaguzi mkuu, kuna kasoro ndogo ndogo ambazo zimejitokeza, hii ni pamoja na baadhi ya wananchi kutoona majina yao kwenye Daftari la wapiga kura, ingawa wanadai kwamba, walijiandikisha. Kuna baadhi ya wananchi hawakufanikiwa kupiga kura hata kama walikuwa wamejiandikisha. Ni kasoro ndogo ndogo zilizojitokeza kwenye uchaguzi mkuu nchini Zimbabwe, lakini mambo yamekuwa ni shwari, dalili za ukomavu wa kisiasa na changamoto ya kukumbatia demokrasia ya kweli.

Wakati huo huo, Bwana Bernard Membe, Waziri wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa kutoka Tanzania ambaye ni mtamzaji kutoka SADC, akizungumza na waandishi wa habari, mwishoni mwa juma, amesema kwamba, uchaguzi mkuu nchini Zimbawe ulikuwa huru na amani. Anawataka wanasiasa nchini Zimbabwe kukubali matokeo rasmi yatakayotangazwa na Tume ya uchaguzi nchini Zimbabwe.







All the contents on this site are copyrighted ©.