2013-08-02 12:12:11

UNICEF: kina mama nyonyesheni watoto wenu!


Tarehe 1 Agosti 2013 ilikuwa ni siku ya kwanza ya Juma la Kimataifa kwa ajili ya kuwahamasisha wanawake juu ya umuhimu wa kuwanyonyesha watoto walio na chini ya umri wa miezi 6.


Shirika la Kuwahudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, (UNICEF) linatoa kipaumbele kwa swala la unyonyeshaji kwani ndiyo njia muafaka ya kuhakikisha afya na maisha ya watoto wachanga yanalindwa na kuokolewa bila ya kutumia fedha nyingi. Kwa sasa ni nusu tu ya watoto walio chini ya miezi 6 wanaofaidika na maziwa ya mama.

Mnamo 2012, ni asilimia 39% ya watoto wote wenye umri chini ya miezi 6 waliobahatika kunyonyeshwa bila kuchanganyiwa vyakula vingine. Hali hii haijapata kubadilika kimataifa kwa karibu ya miaka 20 sasa. Kutokana na mwelekeo wa wanawake wengi kutopenda kuwanyonyesha watoto wao hasa katika nchi zilizoendelea, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendesha kampeni ili wanawake wengi waweze kutambua umuhmu wa kuwanyonyesha watoto wao maziwa ya mama!

Ni dhahiri kwamba, watoto walionyonyeshwa vizuri maziwa ya mama zao wana uwezo mkubwa zaidi wa kuishi katika kipindi cha miezi sita 6 ya kwanza ya maisha yao, ikilinganishwa na watoto wasionyonyeshwa, na kwamba, kuwanyonyesha watoto kuanzia siku ya kwanza ya maisha yao hupunguza kwa asilimia 45% uwezekano wa watoto hao kupoteza maisha yao mapema.

Tarakimu zinaonyesha kwamba nchi kama China ambayo imekuwa mstari wa mbele katika kutumia bidhaa za maziwa ya unga ina asilimia 28% pekee ya wanawake wanaonyonyesha. Hata hivyo, idadi ya watoto wanaonyonya imeongezeka nchini Cambodia kuanzia asilimia 22% kunako mwaka 2000 hadi kufikia asilimia 74% katika kipindi cha Mwaka 2012; Nchi za Togo na Zambia pia zimeonesha ongezeko la idadi ya watoto wanaonyonya kutoka watoto asilimia 20% katika kipindi cha miaka ya 1990 hadi zaidi ya asilimia 60% kuanzia miaka ya 2000.

Nchi za Kiafrika ambazo idadi ya watoto wanaonyonyeshwa imepungua ni pamoja na: Tunisia, Nigeria, Somalia, Chad na Afrika Kusini.

Makamu Mkurugenzi wa UNICEF, Geeta Rao, anasema kwamba, hakuna njia nyingine muafaka, ya kuaminika na rahisi zaidi kuishinda ile ya kuwanyonyesha watoto kutoka kwa mama zao. Kunyonyesha ni kama chanjo ya kwanza kwa watoto, na namna bora zaidi ya kuokoa maisha ya watoto hao, na hasa wale wanaotoka katika familia maskini.

Kuwanyonyesha watoto pia huwakinga na maradhi ya kuwa na uzito wa kupindukia pamoja na magonjwa mengine nyemelezi.
Zaidi ya hayo kunyonyesha huwasaidia akina mama kutopata ujauzito ndani ya miezi sita ya kwanza baada ya kujifungua na kuwakinga akina mama hao na maradhi kama vile saratani ya matiti na ile ya kizazi.

Nchini Italia kuna Hospitali na vitongoji vya afya vijulikanavyo kama Marafiki wa Watoto kwa ajili ya kuwahamasisha akina mama juu ya umuhimu wa kuwanyonyesha watoto wao. Mnamo 2012 watoto 22500 walizaliwa kwenye hospitali hizo 22, na watoto wengine 15400 kwenye vitongoji 2 ambapo kuna huduma za ushauri kwa akina mama ili waweze kulitilia maanani swala la kuwanyonyesha watoto wao, anasema Rais wa UNICEF nchini Italia, Giacomo Guerrera.

Kwa sasa juhudi nyingi zinafanyika ili kuendeleza kampeni hii kwenye maeneo kama vile Abruzzo, Toskana, Veneto, Valle d’Aosta, Sicilia na Milano kama matayarisho ya maadhimisho ya Juma la kimataifa la kuwahamasisha watu juu ya umuhimu wa kunyonyesha watoto, ambalo litaadhimishwa kuanzia Oktoba 1 hadi 7 nchini Italia.
All the contents on this site are copyrighted ©.