2013-08-02 12:12:31

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Waislam wakati wa Maadhimisho ya Siku kuu ya Id El Fitri


Kwa Waislam wote duniani.
Ninayo furaha kubwa kuchukua fursa hii kuwasalimia wakati huu mnapoadhimisha Siku kuu ya Id El Fitri, inayofunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, uliotengwa kwa ajili ya kufunga, swala na sadaka. RealAudioMP3
Ni mapokeo ya siku nyingi kwamba, katika Siku kuu hii, Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini linawatumia ujumbe wa matashi mema, ukiambatana na mada kwa ajili ya tafakari ya pamoja. Mwaka huu, ambao ni mwaka wangu wa kwanza kama Papa, nimeamua kutia sahihi mimi mwenyewe na kuwatumieni, ndugu zangu wapendwa, kama alama ya heshima na urafiki kwa Waislam wote, lakini kwa namna ya pekee viongozi wa kidini.
Kama wengi wenu mnavyofahamu, Makardinali waliponichagua mimi kama Askofu wa Roma na Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki, nilichagua jina la “Francisko” Mtakatifu maarufu aliyempenda Mungu na watu wote, kiasi hata cha kuwaita ndugu zake. Alipenda, akasaidia na kuwahudumia wahitaji, wagonjwa na maskini; ni mtu aliyetunza sana mazingira.
Ninafahamu kwamba, familia na mwelekeo wa kijamii unapata nafasi ya pekee kwa Waislam katika kipindi hiki, ni vyema kutambua kwamba, kuna uwiano wa mambo haya hata katika imani ya Kikristo na utekelezaji wake.
Mwaka huu, mada ambayo ninapenda kutafakari pamoja nanyi bila kuwasahau wote watakaobahatika kuusoma ujumbe huu ni ile inayowahusu Waislam na Wakristo: Kuhamasisha hali ya kuheshimiana kwa njia ya elimu.
Mada ya mwaka huu inapania kufafanua umuhimu wa elimu kadiri tunavyofahamiana, ili kujenga msingi wa kuheshimiana. “Kuheshimiana” maana yake ni mwelekeo wa upendo kwa watu tunaowathamini na kuwajali. Huu ni mchakato wa “pande mbili za shilingi” unaozihusisha pande zote.
Tunachoalikwa kuheshimu kwa kila mtu kwanza kabisa ni maisha yake, mwili wake mzima, utu na haki ambatanishi zinazotokana na utu huo, heshima, mali yake, kabila, utambulisho wake wa kitamaduni, mawazo na msimamo wake wa kisiasa. Tunaalikwa kufikiri, kuzungumza na kuandika kwakuwaheshimu wengine, si tu wakati wanapokuwepo, bali ni kwa daima na kwa wakati wote, kwa kuachana na shutuma au kuwachafulia wengine sifa yao njema. Familia, shule na mafundisho ya dini pamoja na njia za mawasiliano ya kijamii zina dhamana ya kuhakikisha kwamba, lengo hili linafikiwa.
Nikiangalia dhana ya kuheshimiana katika uhusiano wa majadiliano ya kidini, hasa zaidi kati ya Waislam na Wakristo, tunaalikwa kuheshimu dini ya wengine, mafundisho yao, vielelezo vya imani na tunu msingi za maisha ya kiroho. Viongozi wa kidini waheshimiwe pamoja na nyumba za ibada. Inatia uchungu kuona viongozi au nyumba za ibada zinashambuliwa.
Ni wazi kwamba, tunapoheshimu dini ya jirani zetu au pale tunapowatakia wengine matashi mema katika Maadhimisho ya Siku kuu zao za kidini, tunapania kushiriki furaha yao, bila hata ya kufanya rejea kwenye maudhui ya imani yao.
Kuhusiana na elimu kwa vijana wa Kiislam na Kikristo, ni wajibu wetu kuwalea vijana ili waweze kufikiri na kuzungumza kwa heshima kuhusu dini na wafuasi wa dini nyingine, pamoja na kujizuia kuzibeza au kukashifu imani na ibada zao.
Tunafahamu kwamba, kuheshimiana ni msingi wa kila mahusiano, lakini zaidi miongoni mwa waamini wanaoungama imani zao. Kwa njia hii, ukweli na urafiki wa kudumu unaweza kukua.
Nilipokutana na Wanadiplomasia wanaowakilisha nchi zao mjini Vatican hapo tarehe 22 Machi 2013, nilisema, “Haiwezekani kuanzisha uhusiano mwema na Mwenyezi Mungu, wakati unawabeza watu wengine. Kwa hiyo ni jambo la muhimu kuzidisha majadiliano miongoni mwa dini mbali mbali, lakini zaidi na Waamini wa dini ya Kiislam. Katika Ibada ya Misa Takatifu, mwanzo wa utume wangu, nilifurahi kuona viongozi wa Serikali na wa Kidini kutoka katika Ulimwengu wa Waislam.”
Kwa maneno haya, ninapenda kusisitizia kwa mara nyingine tena umuhimu wa majadiliano na ushirikiano miongoni mwa waamini, lakini zaidi kati ya Wakristo na Waislam; jambo linalopaswa kuendelezwa.
Ni matumaini yangu kwamba Wakristo na Waislam watajitahidi kuwa ni vyombo vya kukuza hali ya kuheshimiana na urafiki, hasa kwa njia ya elimu.
Hatimaye, ninapenda kuwatumia sala na matashi mema, ili maisha yenu yaweze kumtukuza Mwenyezi Mungu pamoja na kuwakirimia furaha wale wanaowazunguka. Ninawatakieni Siku kuu Njema ninyi nyote!
Francisko.
Imetolewa Vatican,
Tarehe 10 Julai 2013.All the contents on this site are copyrighted ©.