2013-08-02 08:24:39

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 18 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa


Mpendwa mwana wa Mungu karibuni tena katika kipindi cha tafakari ya Neno la Mungu, ili tushirikishane upendo wa Mwenyezi Mungu kwa njia ya Neno lake lililo hai. RealAudioMP3

Tayari ni Dominika ya 18 ya mwaka C. Mama Kanisa ametuandalia meza ya Neno inayotupeleka kutambua kuwa yafaa kuwa na Hekima katika kutafuta mali na kuwa na mali hizo. Bwana, katika somo la Injili anakuja na neno kali dhidi ya tajiri anayeona aweza kuzuia kifo kwa njia ya mali.

Bwana anasema mpumbavu we! Mhubiri katika somo la kwanza anasema ni ubatili mtupu na Mtakatifu Paulo katika somo la Pili anataka mmoja akishafufuliwa pamoja na Kristo kwa njia ya ubatizo basi daima ayatazame mambo ya juu, yaani kuyacha yale yanayopingana na upendo wa kweli.

Mpendwa msikilizaji, kwa nini huyu ndugu tajiri katika Injili anaonekana kujiweka katika mazingira ya kuridhika na mali akitafuta kujifurahisha na kujiridhisha? Kipi kinampeleka mpaka hapo? Injili haituambii moja kwa moja juu ya kuwa navyo na kuvifurahia! Lakini hebu tuangalie, Bwana anasema mpumbavu we! Usiku huu roho yako itachukuliwa!

Basi maneno ya Bwana yaweza kutusaidia kuelewa kuwa huyu Bwana alikuwa na hofu ya kifo kumbe sasa anaona angalau ajishibishe kwa mali yake akidhani aweza hata kuzuia kifo. Haya ndiyo mawazo yaliyo ya wengi na hasa wazee katika ulimwengu huu. Badala ya kufikiri mambo ya uzima wa milele huanza kufikiria juu ya vitu, nitaviacha namna gani! Mshikamano na vitu hukua na kuongezeka! Bwana anasema mpumbavu we! Leo usiku wanahitaji roho yako.

Mpendwa mwana wa Mungu tuombe kuepukana na tatizo hili la mali. Mali iwe kwa ajili ya mafaa ya wokovu na si kwa mafaa ya kujishibisha na kujenga mshikamano unaoondoa maisha ya mapendo kwa wengine. Tabia hii si ngeni sana katika historia, nakumbuka katika historia ya falsafa, Warumi walikuwa wakisistiza juu ya suala hilo la kujiridhisha na kujifurahisha kwa chakula, kwa sababu ya maisha kuwa mafupi!

Mpendwa maisha yetu ni zawadi, ufupi na urefu si hoja, hoja ni kuishi katika kutimiza mapenzi ya Mungu. Waangalie watakatifu vijana: Dominico Saverio, Gabriele wa Shirika la Wamissionari wa Mateso, Gema Galgani, Theresia wa Mtoto Yesu na wengineo katika ujana yaani ufupi wa miaka yao wamefanya maajabu zawadi za kimungu kwetu.

Mpendwa mwana wa Mungu, Injili inataka kutufundisha utajiri usioogopa kifo, bali utajiri unaoambatana na mapendo makamilifu ya Mwenyezi Mungu. Utajiri unaojikita katika hekima ya kimungu, unaotambua siri ya maisha, unaotambua jumuiya na maisha ya pamoja kinyume na uchoyo anaouonesha tajiri huyu katika Injili.

Injili yataka kadri tunavyosonga mbele katika maisha yetu tunapaswa kukua katika kujitenga na msongo wa mali ili muunganiko na Bwana ukue siku kwa siku na hata siku moja tufurahi pamoja na Kristo mfufuka huko mbinguni. Huu ndio utajiri wa kweli ndiyo maana ya ubatizo wetu.

Nikutakie hekima na heri tele za Bwana siku kwa siku katika maisha yako.
Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.