2013-08-02 10:21:13

Silvio Berlusconi afungwa jela miaka 4 kwa kukwepa kulipa kodi stahiki na kujihusisha na vitendo vya rushwa!


Mahakama kuu ya Italia siku ya Alhamisi, tarehe Mosi Agosti, 2013 imemtia hatiani Bwana Silvio Berlusconi ambaye amewahi kuwa Waziri mkuu wa Italia na mfanyabiashara maarufu nchini Italia kwa kosa la kukwepa kulipa kodi stahiki pamoja na kujihusisha na rushwa.

Kwa makosa haya makuu, Bwana Berlusconi amehukumiwa miaka 4 kwenda jela. Mahakama kuu imetoa amri kwa Mahakama ya rufaa kuangalia jinsi ya kurekebisha utekelezaji wa hukumu iliyokuwa inamnyima haki ya kushiriki katika masuala ya kisiasa kwa miaka mitano. Kwa sasa Bwana Berluscon ataendelea kuwa ni Seneti na Mwenyekiti wa Chama chake cha PDL. Lakini kutokana na umri wake wa miaka 76 anaweza kutumikia kifungo cha nje au kutoa huduma kwa jamii. Bwana Berluscon anasema yeye anatamani kwenda jela.

Kwa hukumu hii, Serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Italia iko mashakani, lakini Rais Giorgio Napolitano wa Italia amewataka wanasiasa kudumisha utawala wa sheria na utulivu kwa ajili ya mafao ya wananchi wa Italia hasa wakati huu ambapo hali bado ni tete katika ujumla wake.All the contents on this site are copyrighted ©.