2013-08-02 09:47:33

Rio 2013 imefunika kwa mengi!


Baba Mtakatifu Francisko alipokuwa anarejea kutoka katika hija yake ya kichungaji nchini Brazil kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani alimshukuru Mungu kwa kufanikisha sherehe hii kubwa ya imani ambayo imeushirikisha umati mkubwa wa waamini na watu wenye mapenzi mema kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Askofu mkuu Oran Joao Tempesta wa Jimbo kuu la Rio de Janeiro akizungumza na waandishi wa habarimapema juma hili, anasema kwamba, Kanisa linamshukuru Mwenyezi Mungu kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 huko Rio de Janeiro. Anasema hata Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, Rio kwa Mwaka 2013 imefunika na kwamba, Kanisa limewahudumia vyema vijana waliohudhuria.

Askofu mkuu Tempesta anasema, ufuko wa Copacabana haujawahi kufurika na watu kiasi hiki, wote hawa wakiwa na amani na utulivu wa ndani, huku wakipania kusikiliza ujumbe uliokuwa unatolewa na Khalifa wa Mtakatifu Petro; wengi wameguswa na wanataka kuona matunda ya Maadhimisho haya yanaleta mabadiliko ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Ni matumaini ya Mama Kanisa kwamba, vijana wa kizazi kipya wataendelea kuwa ni wajenzi wa misingi ya haki, amani na upatanisho miongoni mwa Jamii zao, tayari kujitosa kimaso maso kwa ajili ya kutangaza Injili ya Kristo hadi miisho ya dunia.

Askofu mkuu Tempesta anasema kwamba, zaidi ya watu millioni 3.5 wameshiriki katika Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013. Maadhimisho haya yamefanyika kwenye ufuko wa Copacabana, Quinta da Boa na viunga vya Mji wa Rio. Brazil, Argentina, Marekani, Chile, Italia, Venezuela, Ufaransa, Paraguay, PerĂ¹ na Mexico ni nchi ambazo zilikuwa na wawakilishi wengi zaidi. Bara la Afrika pia liliwakilishwa barabara na makundi makubwa ya vijana; VIjana wa Afrika hawakuvuma, lakini wamo!

Takwimu zinaonesha kwamba, asilia 55% ya mahujaji waliohudhuria walikuwa ni wanawake na wasichana, wakati wanaume na vijana walikuwa ni asilimia 45%. Ndiyo maana hata Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mazungumzo yake na Waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake kwenye hija yake ya kichungaji nchini Brazil alisema kwamba, wanawake wanapaswa kupewa nafasi kubwa zaidi katika kushiriki maisha na utume wa Kanisa, hasa wakati huu wa Uinjilishaji mpya.

Idadi ya mahujaji waliojiandikisha kushiriki katika Maadhimisho ya Siku ya 28 Vijana Duniani inaonesha kwamba, asilimia 60% ya watu wote walikuwa ni vijana wenye umri kati ya miaka 19 hadi 34. Vijana waliojitolea kuwahudumia vijana wenzao kutoka sehemu mbali mbali za dunia walikuwa ni 60,000. Waandishi wa habari waliohakikisha kwamba, watu wanapata kwa wakati muafaka yale yaliyokuwa yanajiri huko Rio walikuwa ni 6,500 kutoka katika nchi 57.

Jimbo kuu la Rio de Janeiro liliandaa vituo 264 vya Katekesi iliyotolewa katika lugha 25 za Kimataifa. Kulikuwa na masanduku 1000 yaliyotumiwa kwa ajili ya Sakramenti ya Upatanisho. Maaskofu waliohudhuria walikuwa ni 644 na kati yao kulikuwa na Makardinali 28. Mapadre walikuwa ni 7, 814 na Idadi ya Mashemasi ilikuwa ni 632. Takwimu za uchumi zilizotolewa na Wizara ya Utalii zinaonesha kwamba, watu wametumia kiasi cha dolla za kimarekani millioni 780 wakati walipokuwepo nchini Brazil.All the contents on this site are copyrighted ©.