Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na mafanikio ya Benki ya Mkombozi
Benki ya Mkombozi ambayo ni tunda na juhudi za Kanisa Katoliki katika kumkomboa mtanzania
wa kawaida kwa kumjengea uwezo wa kiuchumi inaendelea vyema. Kwa kipindi cha miaka
mitatu na nusu tangu ifunguliwe imekwisha fungua matawi manne.
Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania linamshukuru Mwenyezi Mungu kwa mafanikio yote yaliyokwisha
kupatikana katika kipindi.
Maaskofu wanawaomba wale walionunua hisa zao kwenye
Benki ya Mkombozi kuvuta subira, kwani mchakato wa kufungua matawi mapya umekwamisha
kidogo zoezi la kuanza kugawana faida. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linasema,
kuwa na matawi mapya ni faida, kwani Benki ya Mkombozi itaweza kutoa huduma kwa watu
wengi zaidi. Lengo la Benki hii ni kuhakikisha kwamba, inafika Tanzania nzima kwa
haraka iwezekanavyo!
Hii ni sehemu ya barua iliyoandikwa na Askofu Tarcisius
Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania akiwataka waamini na wote
walionunua hisa katika Benki ya Mkombozi, kujifunga kibwebwe ili kuweza kukabiliana
na changamoto iliyotolewa hivi karibuni na Benki kuu ya Tanzania kwa kuagiza kwamba,
Mabenki yote nchini kuongeza hisa zake kutoka Billioni tano, Kiwango cha sasa hadi
kufikia Billioni kumi na tano.
Baraza la Maaskofu linawaomba waamini na watu
wote wenye mapenzi mema kuona kwamba, Benki ya Mkombozi ni chombo makini cha kuwalatea
watanzania maendeleo endelevu na kwamba, wanapaswa kuonesha uzalendo kwa kuchangia
kwa hali na mali katika harakati za kufanikisha ongezeko la mtaji. Jambo hili linawezekana
kwa kununua tena hisa kutoka katika Benki ya Mkombozi, kwa mtaji mkubwa zaidi, pengine
kuliko ilivyokuwa hapo awali.
Mama Edwina Lupembe, Mkurugenzi mtendaji wa Benki
ya Mkombozi ameanza zoezi ka kuhamasisha upatikanaji wa mtaji huu kutoka sehemu mbali
mbali za Tanzania. Baraza la Maaskofu Katoliki linawaalika waamini na watu wenye mapenzi
mema kuonesha moyo wa ushirikiano, ili kufanikisha zoezi hili.
Wadau wajijengee
utamaduni na mazoea ya kutumia huduma mbali mbali zinazotolewa na Benki ya Mkombozi:
kwa kuweka na kukopa pamoja na kuwaalika marafiki, ndugu na jamaa kujiunga na Benki
ya Mkombozi.
Itakumbukwa kwamba, Benki ya Mkombozi inatoa pia huduma za fedha
za kigeni, kumbe watu wanaweza kuitumia kwa kuzingatia maelezo ya utumaji wa fedha
za kigeni kwa kupitia Benki ya Mkombozi.